Wednesday , 8 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lowassa, Sumaye wamtia gundu Membe
Habari za Siasa

Lowassa, Sumaye wamtia gundu Membe

Spread the love

WASWAHILI husema ‘ukiumwa na nyoka, ukigusa jani unashtuka,’ hiki ndicho kinachomtokea Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya nne. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua ya Edward Lowassa na Frederick Sumaye, mawaziri wakuu wastaafu kutoka chama cha upinzani – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemtia nuksi na kumweka kwenye wakati mgumu Membe.

James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi anaungana na vyama vingine, kuonesha hofu ya kumpokea Membe iwapo atataka kujiunga na chama hicho.

Akizungumza na wahariri waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communication (CML), jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Machi 2020, alipoulizwa kama chama chake kiko tayari kumpokea Membe iwapo atataka kujiunga na nacho, Mbatia amesema lazima kuwe na umakini.

Mbatia ameeleza wazi, kwamba kilichofanywa mwaka 2015, wakati walipomkaribisha na kumruhusu Lowassa kujiunga na kisha kugombea urais, akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kinatakiwa kutotokea tena.

Amemtaja Lowassa na Sumaye kama mfano mbaya ambao wapinzani wanapaswa kujifunza, na kwamba ndio msingi wa kumuhofia Membe.

“Makosa ya 2015 ya kina Lowassa, Sumaye na wengine yawe mafundisho tosha kwetu sisi,” amesema Mbatia na kuongeza, kwamba kumpokea mtu na kuwa mwanachama, anakuwa na haki zote hivyo lazima umakini uwepo.

Lowassa alijiunga na Chadema Julai 2015, huku ikielezwa kwa masharti ya kuteuliwa na kugombea urais jambo ambalo lilitekelezwa na kuacha mpasuko mkubwa ndani ya vyama vya upinzani.

Lowassa alitangaza kurejea CCM tarehe 1 Machi 2019, ambapo Sumaye alitangaza kurejea kwenye chama hicho tarehe 10 Februari 2020.

Miongoni mwa wanaoonesha mashaka ya kumpokea Membe ni pamoja na Maalim Seif Sharif Hamad, Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Maalim Seif alisema, Membe kama anataka kujiunga na chama hicho, hapaswi kwenda na masharti kama ilivyotokea kwa Lowassa mwaka 2015.

Maalim Seif alisema “Membe? Sie tunapokea yeyote atakayekuja, asije na masharti, tunampokea.”

Mzee Hashimu Juma, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (BAZECHA), tarehe 3 Machi 2020 alisema Chadema kimeweka matumaini yake kwa Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa chama hicho kugomea urais kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mzee Juma alimshauri Membe kujiunga na chama kingine cha upinzani ili kupunguza kura za CCM, huku akitamba kwamba hawezi kupunguza kura za Chadema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!