Thursday , 9 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu ashangaa wadhamini wake
Habari za SiasaTangulizi

Lissu ashangaa wadhamini wake

Spread the love

SIKU moja baada ya wadhamini wa Tundu Lissu katika kesi ya tuhuma za uchochezi kupitia gazeti la MAWIO, kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa hati ya kumkamata, mwwenyewe amesema, hata ikitolewa ni ngumu kutekelezwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).  

Amesema kilichofanywa na wadhamini wake Robert Katula na Ibrahim Ahmed ni kutengeneza vichwa vya habari vya magazeti kwa siku mbili-tatu, na kwamba anasikitika wadhamini wake kuchukua hatua hiyo.

Amesema inawezekana kuwa wadhamini hao huwenda wamechoka lakini labda pia wamesukumwa kuchukua hatua hiyo.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Februari 2020, kwenye mahojiano na waandishi wa Mwanahalisi Online.

Alipoulizwa kama ikitokea hati hiyo kutolewa itamuathiri kwa kiwango gani, Lissu amesema “sidhani kama kuna madhara yoyote ya kutoa amri ya kunikamata zaidi ya kutengeneza vichwa vya habari vya magazetini na mitandaoni kwa siku mbili au tatu.”

Kwenye kesi hiyo ya uchochezi Na. 208/2016, mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni Simon Mkina, mhariri wa gazeti la MAWIO; Jabir Idrissa, mwandishi wa gazeti hilo na Ismail Mehboob, meneja wa kampuni ya uchapishaji ya Flint.

Wote wanne, wanatuhumiwa kuandika, kuchapisha na kusambaza taarifa hizo kwenye gazeti la MAWIO la tarehe 14 Januari 2016, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002 ambayo ilishafutwa na kutungwa sheria mpya Na. 12 ya mwaka 2016.

Habari iliyotumika kutengeneza mashitaka hayo ilikuwa na kichwa cha habari Maafa yaja Zanzibar.

Pia wanatuhumiwa kuchapisha habari hizo kwa lengo la kueneza chuki kwa wananchi wa Zanzibar, kuchapisha gazeti la MAWIO la Januari 13, 2016 na la nne la kuchapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti wa Serikali, yanamhusu Mehboob ambaye ni Meneja wa kampuni ya uchapishaji ya Flint.

Shitaka la tano ni la kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar, ili wasiweze kuingia kwenye uchaguzi wa marudio linawahusu washitakiwa wote.

Hata hivyo, Lissu amesema wadhamini wake waliwasiliana naye pale walipochukua hatua, na kwamba alifahamu kwa undani wake hatua ya wadhamini hao kufikia hatua hiyo.

Ombi la wadhaminiwa wa Lissu kutaka hati ya kukamatwa kwake lilifahamika jana tarehe 20 Februari 2020, kupitia kwa Wakili wa Serikali anayewakilisha upande wa mashitaka, Wankyo Simon alipoieleza mahakama kuwa anaomba suala hilo lipangiwa siku ya kusikilizwa.

Mahakama iliahirisha kesi hadi leo ambapo Hakimu Simba aliamua ombi hilo lije kusikilizwa tarehe 10 Machi kufuatia ombi la Wakili Wankyo kutaka muda zaidi wa kushughulikia hati ya kiapo ya majibu ya maelezo ya kwenye kiapo cha waombaji – wadhamini wa Lissu.

Washitakiwa wote wanaendelea na dhamana. Hata hivyo, kutokuwepo nchini kwa Lissu ambaye amekuwa ughaibuni tangu alipokwenda kwa matibabu ya majeraha ya risasi aliposhambuliwa tarehe 7 Septemba 2017, kumesababisha kibano kwa wadhamini wake kuwa wamlete afike kesi inapoitwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Kuanzia Agosti marufuku kutumia mkaa, kuni

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mwendokasi Kigogo – Segerea kujengwa awamu ya 5

Spread the loveNaibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Festo Dugange...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

error: Content is protected !!