Wednesday , 8 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CCM Mwanza watifuana, maslahi binafsi yatajwa
Habari za SiasaTangulizi

CCM Mwanza watifuana, maslahi binafsi yatajwa

Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire. Picha ndogo, Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
Spread the love

VIONGOZI wakubwa wa Jiji la Mwanza, James Bwire, Meya wa jiji hilo kwa tiketi ya CCM na Mkurugenzi wa jiji hilo, Kiomoni Kibamba ambaye ni kada wa CCM, wameingia katika vita baridi huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake, anaandika Moses Mseti.

Mkurugenzi Kibamba anamtuhumu Meya Bwire kwa kujitwalia eneo la heka saba za ardhi ambazo ni mali ya jiji hilo na kuanza ujenzi wa hospitali yake binafsi bila kufuata taratibu, kanuni na sheria za ujenzi na kudai eneo hilo ni mali halali ya jiji huku akitumia nafasi yake kumiliki eneo hilo.

Tuhuma hizo za Mkurugenzi Kibamba ni kujibu mapigo baada ya kutuhumiwa na Meya Bwire aliyoongoza Kamati ya Fedha na Uongozi kukakua mradi wa uboreshaji miundombinu na kugundua kuna mapungufu kwa kujengwa chini ya kiwango huku wakidai mkurugenzi anamiliki kampuni zilizopewa zabuni.

Kinachoonekana Aprili 23 – 24 mwaka huu, Meya huyo pamoja na Kamati ya Fedha na Uongozi ya Jiji la Mwanza walipofanya ziara katika mradi wa uboreshaji miundombinu ya takataka kwenye dampo la Buhongwa linalojengwa kwa zaidi ya Sh. 450 milioni walibaini mradi upo chini ya kiwango na hauendani na thamani halisi ya fedha iliotolewa.

Tuhuma hizo ziliibuliwa na mkurungezi huyo wakati alipofika eneo hilo lililokuwa limetengwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na shule na matumizi mengine ya umma kwa kata ya Mahina ambayo meya Bwire ni diwani.

Kibamba akizungumza mara baada ya kufika eneo hilo na kusitisha ujenzi wa jengo hilo la hospitali, alidai kwamba meya huyo badala ya kusimamia sheria, amegeuka chanzo cha uvunjaji wake na kusababisha migogoro.

Amesema kuwa anashangaa kuona meya huyo aking’ang’ania eneo hilo na kuanza ujenzi huku akifahamu fika eneo hilo ni mali ya serikali, kitendo ambacho alidai kwamba kiongozi huyo anatumia vibaya madaraka yake kwa ajili ya kujinufaisha.

Kibamba amesema kuwa baada ya kuibuka kwa mgogoro huo mwaka 2013 walianza kufanya uchunguzi na kutafuta nyaraka za eneo hilo na kubaini eneo hilo lilitwaliwa 2002 na serikali ya mtaa.

Amesema katika kipindi hicho, vielelezo vilionesha kwamba mwaka 2009 wananchi 37 waliokuwa wanamiliki eneo hilo walilipwa fidia kupisha eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya umma lakini wanashangaa kuona meya huyo akiibua mgogoro huo na kudai ni mali yake.

Kibamba aliendelea kueleza kwamba wakati mgogoro huo umepamba moto, ukiongozwa na meya huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shule ya Alliance ya jijini hapa, walianza kushughulikia tatizo hilo.

Hata hivyo, Kibamba alidai kwamba, wakati wanaendelea kushughulia tatizo hilo, Aprili 4 mwaka huu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi alipofanya ziara kwenye kata ya Mahina, baadhi ya wananchi walijitokeza kulalamika kuhusu eneo hilo.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo, waziri Lukuvi alimuagiza mkurugenzi na wataalamu wake kufanyia kazi suala hilo ambapo walibaini mgogoro huo unasukwa na meya ili aweze kujenga hospitali yake binafsi jambo ambalo limedhihirika hivi sasa.

Pia Kibamba alidai kwamba baada ya kubaini chanzo cha mgogoro huo ni meya, walizungumza nae lakini yeye aligoma kutoa ushirikiano na kugeuka ‘mbogo’ na wao wakaachana nae na kutafuta njia nyingine ya kuushughulikia

“Wakati tunaendelea na mgogoro huo, kama agizo la waziri lilivyotolewa (Lukuvi) lakini tulishangaa yeye (Meya) ameanza kupeleka vifaa eneo hilo na kuanza ujenzi na tulimwambia asitishe zoezi hilo lakini alikaidi.

“Mei 7 tilimumpa zuio la kujenga eneo hilo lakini hakutaka kutusikiliza na akaendelea kujenga na wakati anaendelea, leo (juzi) tumefika hapa kuzuia ujenzi na kuweka alama ya x mpaka mgogoro utakapoisha na kama eneo ni lake ataliendeleza,” amesema Kibamba na kuongeza:

“Yeye ndio tulizani atakuwa mstari wa mbele katika kulinda maeneo ya jamii lakini yeye sasa amekuwa ndio mstari wa mbele kuibua mgogoro huu na hatuwezi kukubali lazima mambo kufanywa bila taratibu ni lazima sheria ifuatwe.”

Kwa upande wake Meya huyo ambaye wakati mkurugenzi huyo aliyeambatana na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Marry Tesha kwenda kuzuia zoezi la ujenzi huo kusimamishwa aligoma kuzungumzia suala hilo na kugoma hata kupigwa picha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the loveTAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Spread the loveWAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mabeyo ametuepusha

Spread the loveNIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa...

Habari za SiasaTangulizi

CCM yaitaka TAKUKURU kuichunguza Chadema tuhuma alizoibua Lissu

Spread the loveCHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana...

error: Content is protected !!