
Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani, akiangalia athari zilizotokana na mapigano ya wakulima na wafugaji
MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) ameitaka serikali kueleza namna ilivyojipanga kupambana na janga la mapigano baina ya wakulima na wafugaji, anaandika Dany Tibason.
Akiuliza swali bungeni leo, mbunge huyo amesema mapigano hayo yamekuwa yakisababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
“Je, serikali imejipangaje kupambana na janga hili?” alihoji Kikwete
Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alikiri kuwepo kwa migogoro hiyo kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo kadhaa ndani ya nchi ambayo yamesababisha watanzania kupoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo serikali kupitia jeshi la polisi inaendelea kushauri mamlaka zinazosimamia matumizi bora ya ardhi kutenga maeneo yatakayotumiwa na wakulima na wafugaji ili kuepusha migogoro hiyo.
Lakini pia Nchemba amesema serikali inatoa elimu kwa wakulima na wafugaji juu ya matumizi bora ya ardhi.
“Aidha jeshi la polisi hufanya doria na misako na kukamata mifugo inayoingia katika mashamba ya wakulima vitendo ambavyo vinasababisha migogoro ya mara kwa mara na kuhatarisha amani,” amesema Nchemba.
More Stories
Dk. Mpango azitaka mamlaka maliasili utalii kukomesha urasimu vibali
TANESCO yaghairi matengenezo mfumo wa LUKU
Morogoro yapokea bilioni 111 miradi ya maendeleo