July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Safari matumizi ya Kiswahili mahakamani yaanza

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma

Spread the love

 

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba amesema, wizara yake imezungumza na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa ajili ya kurekebisha sheria inayozuia matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika sheria na shughuli za mahakama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Nchemba ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 2 Februari 2021, katika hafla ya uapisho wa Zepharine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, iliyofanywa na Rais John Magufuli, Ikulu ya Chamiwno, jijini Dodoma.

Galeba aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, alipandishwa cheo na Rais Magufuli jana Jumatatu tarehe 1 Februari 2021, baada ya kutumia Lugha ya Kiswahili katika Kesi ya mapitio Namba 23/2020 ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi.

 

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya AG kufanya marekebisho ya sheria ili lugha ya Kiswahili itumike katika shughuli za mahakama na sheria.

Akizungumzia agizo hilo, Dk. Nchemba amesema, wizaya yake ilifuatilia suala hilo na kugundua, kulikuwa na sheria inayoelekeza lugha ya sheria na mahakama kuwa ya Kingereza.

Hivyo, ameongea na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adelardus Kilangi ili taratibu za kurekebisha sheria hiyo zianze.

“Sisi kama wizara, tumefuatilia tukagundua kulikuwa na sheria inaelekeza hivyo, kwamba lugha ya sheria na mahakama itakuwa Kingereza. Tumeongea na mwanasheria mkuu aweze kutuongoza tuweze kurekebisha,” amesema Dk. Nchemba.

Dk. Nchemba amesema, wizara yake pia ilifanya majadiliano na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kwa ajili ya suala hilo, ambaye alisema hana pingamizi juu ya mabadiliko hayo.

“Katika kutekeleza malekezo haya, namshukuru Jaji Mkuu hata kwenye mjadala tuliokuwa tunafanya moja kwa moja, alisema mzigo hauko kwake uko wizarani. Kwamba tukibadilisha hayo yeye hana pingamizi,” amesema Dk. Nchemba.

Awali, Rais Magufuli aliiagiza wizara hiyo kupitia kwa AG kufanya mabadiliko ya sheria zinazozuia Kiswahili kutumika mahakamani.

“Kama AG anatoka wizara hiyo, mmeshinda kitu gani kufanya amendment (amerekebisho)? AG kila siku anafanya amendment za wizara nyingine, za wizara inayomhusu hafanyi.”

“Sasa niwaombe wahusika wote wa wizara sababu saa nyingine lawama hizi zinapelekwa kwa majaji wakati wala hawahusiki, ni kutokana na hii sheria ambayo ilipelekwa na watu waliopenda Kingereza wakati huo,” amesema Rais Magufuli.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisema, hoja za kuwa Kiswahili hakina misamiati ya kutosha hazina mashiko kwa kuwa mwaka 1999, timu ya wanasheria iliandika kamusi ya sheria na pia lugha hiyo inatumiwa na watu wengi, mataifa na taasisi mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari vya kimataifa.

error: Content is protected !!