SHIRIKA la Viwango Tanzanianchini (TBS), limeeleza linatengeneza mfumo imara ili kuhakikisha, magari yote yatakayoingizwa nchini yanakuwa na viwango stahili. Anaripoti Brightness Boaz, Dar es Salaam … (endelea).
Roida Andusamile, msemaji wa TBS ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 2 Februari 2021, baada ya kuulizwa na MwanaHALISI Online kwamba, serikali itasaidiaje kuokoa gharama za muagizaji gari iwapo litaingizwa nchini bila kuwa na viwango stahili.
Pia, MwanaHALISI Online lilitaka kujua iwapo, serikali imeweka mfumo imara kuhakikisha kampuni za uuzaji magari haziuzii Tanzania magari yasiyo na viwango hivyo kumuingiza gharama mnunuzi.
Roida amesema, kabla ya mfumo mpya wa uagizaji magari kuanza, TBS itakaa na mawakala wa kampuni wanaoagiza magari na kuwaeleza namna ya kukwepa kuwaingiza gharama wateja wao.
“Tunatarajia kukaa na mawakala kabla ya ukakuzi kuanza ili kuwaeleza namna utaratibu utakavyokua, hivyo basi wasiwe na wasiwasi wowote,” amesema.
Msemaji huyo amesema, shirika ili litakutana na mawakala hao ili kueleza zaidi namna mfumo huo mpya utakavyokuwa na manufaa kwao na kwamba, iwapo watakuwa na maswali basi watapata fursa ya kujibiwa.
Pia, amewataka wananchi kuwatumia mawakala wanaotambulika waweze kuagiza magari ili waweze kukaguliwa nchini.

“Hii ni faida kwa wananchi pia kwa wafanyabiashara wa magari, watanufaika zaidi, tofauti na ambavyo kila mtu anaagiza gari anavyojua yeye.
“Sasa hivi itakua salama zaidi kutumia kampuni zilizopo hapa nchini kuagiza magari, na kuwa na uhakika wa gari inayoingia nchini ni ya aina gani,” amesema Roida.
Amesema, TBS baada kumaliza mkataba wake tarehe 28 Februari 2021 na kampuni za nje zinazohusika kukagua magari, haitaingia mkataba nao tena na badala yake, watawatumia mawakala wa kampuni zinazojulikana hapa nchini kuagiza magari hayo ili waweze kuyakaguwa.
“Kwanzia tarehe 1 Machi 2021, TBS tutaanza ukaguzi na watakao faidika zaidi ni mawakala wa makampuni ambayo yanajulikana,” amesema Roida.
Leave a comment