Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nenda Jaji Augustino Ramadhani, umefanya yaliyokuhusu
Habari za SiasaTangulizi

Nenda Jaji Augustino Ramadhani, umefanya yaliyokuhusu

Spread the love

KASISI wa Kanisa la Anglikana Visiwani Zanzibar, Jaji Augostino Ramadhani (74), ameaga dunia. Amekutwa na mauti jana Jumanne, katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam. Mpaka sasa, naandika makala hii, ilikuwa haijaelezwa kilichosababisha mauti yake. Anaandika Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa WhatsApp na ambayo inadaiwa kuandikwa na Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma iliishia kusema, “Jaji Ramadhani amekutwa na mauti muda mfupi uliyopita.”

Nilibahatika kumfahamu kidogo Jaji Ramadhani. Nilikutana naye kwenye midahalo mbalimbali. Hakuwa na majivuno. Alikuwa msomaji mzuri wa magazeti yetu ya MwanaHALISI na MAWIO. Mara kadhaa alikuwa akinipigia simu kukosoa au kusifia baadhi ya makala na habari tulizozichapisha. Hakika, alinivutia, na kwangu alikuwa kiongozi wa aina yake.

Niliwahi kufanya naye mahojiano mara nyingi. lakinininazoweza kuzikumbuka sana, ni pale alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano; alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na alipotawazwa kuwa Kasisi wa Kanisa lake la Agrikana.

Mbali na kustaafu ujaji, alipewa kazi ya ukasisi, alitawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar, Desemba 2013 na hivyo kustahili kuitwa cheo cha Mchungaji Augustino Ramadhani.

Mchungaji Augustine alizaliwa tarehe 28 Desemba 1945, Kisima Majongoo, kisiwani Zanzibar, kutoka familia ya watoto wanne wa Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Anna Constance Masoud, akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo.

Aliishi Zanzibar kwa miaka mitatu na kisha alikuja Tanzania Bara (Tanganyika) akiwa na umri wa kuanza masomo hadi alipohitimu masomo ya sekondari katika Shule ya Wavulana Tabora na wakati akiwa sekondari ndipo alipojifunza kupiga kinanda akirithi kipaji cha babu yake Augustino Ramadhani.

Jaji Ramadhani alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1965 na kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika fani ya sheria hadi mwaka 1970 alipojiunga katika Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, baadaye aliajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) alikofanya kazi za sheria.

Mwaka 1978 aliitwa na aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe, kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwaka huo huo aliitwa tena jeshini kwa ajili ya kushiriki vita ya Kagera. Alipelekwa Uganda na kukaa kwa zaidi ya miezi kumi.

Alijiunga na jeshi kama mwanasheria raia, hadi alipopata mafunzo ya kijeshi na baadaye kuwa afisa wa jeshi hilo. Mwaka 1971 alitunukiwa nyota mbili (Luteni). Aliendelea na kazi ya jeshi hadi mwaka 1977, alipohamishiwa Brigedi ya Faru-Tabora akiwa na cheo cha Meja.

Akiwa Uganda ambako sasa alikuwa tayari na cheo cha Luteni Kanali, aliendesha mahakama za kijeshi. Vita ilipomalizika alirudi Tanzania kuendelea na kazi katika sekta ya Sheria na tarehe 8 Januari 1980, aliitwa tena na Rais Jumbe na kuapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Alishika nafasi hiyo, hadi Septemba 1989. Alistaafu jeshi mwaka 1997 akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali.

Kipindi Jaji Ramadhani akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu waZanzibar, bosi wake, alikuwa Jaji Damian Lubuva.

Augustino Ramadhani  amewahi kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Jaji Mkuu waJamhuri ya Muungano, Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jaji wa Mahakama ya Rufani na makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC).

Pia aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka 1989, mwaka 1990 alihamia jijini Dar es Salaam na mwaka 1993 hadi 2003 aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Bara na mnamo mwaka 2002-2007 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Alikuwa mmoja wa majaji sita wa mahakama ya Afrika Mashariki, pia alikuwa ni mmojawapo wa Majaji 11 waliochaguliwa na Marais wa Afrika kwa ajili ya kuitumikia Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na ndipo tarehe 17 Julai mwaka 2007, alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI, siku moja baada ya kuapishwa kuwa Jaji Mkuu, Jaji Ramadhani alisema, alilenga kupambana na rushwa iliyokithiri katika sekta ya mahakama.

Hata hivyo, Jaji Ramadhani baadaye alikiri kuwa ukwapuaji wamabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow na “mgawo” waliopata baadhi ya majaji, vilitibua rekedi yake.

“Watu wanaweza kusema, haya yametokana na mfumo mbaya wa mahakama au niliyouasisi au kuuendeleza,” alieleza.

Akizungumzia mfumo wa Mahakama Visiwani, Jaji Ramadhani alisema, haukuwa wa kisheria na alifanikiwa kuubadilisha na kuweka mfumo wenye ngazi za kimahakama kutoka wilaya, mkoa hadi mahakama kuu.

Alibainisha kuwa hii ilitokana na kutokuwepo na watu waliosomea sheria ili kuajiriwa katika sekta ya sheria.

“Nilifanikiwa kuondoa mfumo wa mabaraza (Peoples Court) na kuweka mfumo wa mahakama uliofuata ngazi za kimahakama na mahakama ya Rufaa haikuwepo kabisa”, alinieleza.

Baada ya kustaafu kazi ya ujaji mkuu mwaka 2010, Jaji Ramadhani alikataa kuendelea na kipindi kingine baada ya kufanikiwa kufafanua kifungu kinachokataza Jaji kuendelea na kazi ya ujaji baada ya umri wake wa kustaafu na kuendelea kwa mkataba wa ajira, ila anaruhusiwa kuongeza kipindi kimoja tu hata kama bado anazo nguvu za kutumikia taifa.

Hata hivyo, utumishi wake uliotukuka katika muhimili huo sheria, uliingia doa kufuatia maamuzi ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa, yeye akiwamo, kutupilia mbali suala la mgombea binafsi.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Ramadhani alisema, mahakama hiyo haina mamlaka ya kuamua juu ya hoja ya mgombea binafsi kwakuwa ni suala la kisiasa na akashauri Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kulitafutia ufumbuzi.                    

Kesi hiyo, ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye aliiomba mahakama kubatilisha kipengele kinachozuia mgombea binafsi. Alisema, sheria hiyo inakiuka Katiba.Maamuzi haya yalifanyika Juni mwaka 2010.

Majaji wengine waliokuwamo kwenye kesi hiyo, ni Jaji Eusebio Munuo, Januari Msofe, Benard Luanda, Mbarouk Mbarouk, Nathalia Kimaro na Sauda Mjasiri.

Miongoni mwa waliotilia shaka uamuzi huo, ni aliyepata kuwa Jaji Mkuu Barnabas Samatta. Baada ya kusikia hukumu ile, Jaji Samata alisema, “imeonyesha dhahiri kuwa mhimili huo unayumbishwa na wanasiasa.”

Jaji Samatta alisema, “…ninachojua ni kwamba malalamiko yoyote yanayohusu mabadiliko ya kifungu chochote cha katiba au kuamua kuhusu haki kwenye uchaguzi ni suala la kisheria na si jambo tu tunaloweza kulielezea ni la kisiasa.”

Akaongeza, “hebu tujaribu kukubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuwa suala la mgombea binafsi lilikuwa la kisiasa. Mtazamo huo nafikiri utamfanya mtu kujiuliza.

Kwa nini mahakama iliamua kujiingiza katika jambo hili la kisiasa hata kutoa ushauri kwa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali namna ya kuamua mambo ya siasa?”Jaji Ramadhani ndiye aliyemrithi Jaji Samatta. 

Jingine lililotia doa utumishi wake, ni uamuzi wake wa kujitosa katika katika mbio za urais, Juni 2015.

Kasisi huyo aliondoka katika kituo chake cha kazi, Mkunazini, Unguja na kuelekea moja kwa moja mkoani Dodoma, kuchukua fomu ya kugombea urais, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mchungaji Ramadhani hakusita kuzungumzia suala la rushwa, ambalo limezungumziwa na takribani kila mwanachama wa chama hicho, aliyechukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Nilipomuuliza kama ana ubavu wa kupamba na rushwa ambayo tayari imeota mizizi nchini, hara alinieleza, “nilipokuwa mahakamani nilifanya kazi hiyo.”

Nilipomueleza kuwa haoni kushindwa kwake kupambana narushwa katika sekta ya mahakama kunamuondolea sifa ya kuwa mgombea, Jaji Ramadhani alinijibu:

“Chema chajiuza, kibaya chajitembeza. Nina sifa zote za kuongoza Tanzania,” alisema na kuwatambulisha watoto wake na ndugu wa familia yake akisema, “nimekuja nao hawa tu sitaki mbwembwe kama wengine wanavyofanya.”

Alisema, anavyo vigezo vyote vya kushika wadhifa huo kikiwemo cha uzoefu wa uongozi kwa kuwa alitumikia jeshi kufikia ngazi ya Brigedia Jenerali. 

 Aliongeza: “Nikijaliwa kuwa rais, sheria zipo tutazitekeleza kukabiliana na rushwa.”

Jaji Ramadhani anatajwa kuwa alikuwa mtu safi kabisa kuhusu mambo ya rushwa na ufisadi.

Augustino Ramadhan alisema alijiunga tena na CCM, Septemba mwaka 2011, katika tawi la chama hicho, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Kauli yake juu ya uwanachama wake wa CCM, ilizua utata mkubwa. Baadhi ya wachambuzi walisema, hatua ya Jaji Ramadhani kugombea urais kupitia CCM, ni ushahidi kwamba alikuwa mwanachama wa chama hicho, wakati akiwa jaji mkuu. Wapo waliohusisha mbio zake hizo za urais na maamuzi aliyofanya kwenye kesi ya Mtikila.

Amesema yeye aliingia katika CCM mwaka 1969 wakati akiwa mwanafunzi wa shahada ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mara baada ya kusimikwa kuwa Mchungaji alisema, hakuna tofauti kati ya kazi ya Mahakama na kazi ya Uchungaji kwani zote ni kazi za kufanya maamuzi ya watu wanaodai wapatiwe haki na kubainisha kazi za mahakama ukiamua umeamua ila za kanisa zinataka makubaliano na maridhiano japo zote ni kazi za Mungu.

“Kazi hii ya uchungaji mimi sikuifikiria hata siku moja kwamba nitaifanya ingawa nilisomea nchini Uingereza na kutunukiwa stashahada. Pia nilikuwa nikishiriki katika shughuli za madhabahuni hasa wakati wa kuwasimika maaskofu kwa kuwa nilikuwa mwanasheria wa kanisa hili hadi nilipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu ndipo nilipoamua kuacha wadhifa huo ili kuepuka migongano wa maslahi,” alinieleza.

Kwa upande mwingine, Jaji alisema, lengo lake lilikuwa baada ya kustaafu akafundishe na lengo hilo lilitimia kwani alipata kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Tumaini Iringa alikokuwa anafundisha sheria.

Pia atakumbukwa kwa kazi nzuri ya kukamilisha uundaji warasimu mpya ya katiba, ingawa amekufa bila kuona Katiba Mpya.

Brigedia Jenerali Augustino Ramadhani alifunga ndoa na mke wake wa kwanza, Luteni Kanal Saada Mbarouk, ambaye alikuwa mfanyakazi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Makao Makuu jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Novemba 1975

Mwandishi wa makala haya, Saed Kubenea, ni mkurugenzi mtendaji na mhariri mtendaji wa magazeti ya MwanaHALISI, na mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwasimu Na. 0782072292

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!