October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yapokea msaada wa Bil 14.9

Spread the love

SERIKALI imepokea msaada wa Sh. 14.9 bilioni kutoka Global Fund, Airtel Tanzania, Rotary Club Tanzania ambazo sehemu kubwa zitatumika kununua vifaa kinga kwa watumishi wa afya na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye maambukizi ya COVID-19. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Msaada huo umepokelewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ikiwa pamoja na lita 1,250 za vitakasa mikono ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Waziri Ummy amefafanua kwamba Global Fund imetoa Sh.14 bilioni, Airtel Tanzania Sh. 700 milioni na Rotary Club Tanzania wametoa Sh. 250 milioni.

“Tumepokea Sh. 14 bilioni kutoka Global Fund, Sh. 9.6 bilioni tumezitoa kwa ajili ya kununua vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa Afya, lakini pia fedha zilizotolewa na Airtel na Rotary Club Tanzania tutazielekeza huko. Kipaumbele chetu ni kuwalinda watumishi wa afya,” amesema Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

“Natumia fursa hii kuwashukuru watumishi wa afya ambao wamekuwa wakijitoa usiku na mchana katika kutoa huduma kwa watu waliopata maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19) pamoja na wale wahisiwa.

“Kipaumbele cha Serikali ni kuwalinda watumishi wa Afya kwa kununua vifaa kinga kwani fedha tulizozipata hapa tutazielekeza kwenye ununuzi wa vifaa kinga. Niendelee kuwaisistiza Watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya magonjwa ya kuambukiza,” amesema Waziri Ummy.

Amesema watumishi wa afya ambao wamepatiwa mafunzo katika vituo vya kutoa huduma kwa wenyr maambukizi ya ugonjwa huo, hakuna aliyepata maambukizi kwa kuwa wanazingatia miongozo ya Serikali ya kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Covid-19 pamoja na miongozo ya magonjwa ya kuambukiza.

Waziri amesema ushiriki wa kila mdau katika mapambano dhidi ya maambikizi ya virusi vya Corona ni muhimu na kwamba msaada uliotolewa na kampuni hizo ni mkubwa katika mapambano ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

“Napenda kurudia tena kwa niaba Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, nawashukuru Airtel Tanzania, Serengenti Breweries na Rotary Club kwa hiki mlichotupatia. Asanteni sana,” amesema Waziri Ummy.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Airtel Tanzania, Gabriel Malata amesema Airtel Tanzania imetoa Sh. 700 milioni ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la Corona.

“Sisi bodi ya wakurugenzi wa Airtel na kwa niaba ya Airtel Tanzania, tunatambua juhudi za Serikali katika kupambana na ugonjwa wa Corona, lakini pia tumejitathimini na kutambua kuwa sisi kama Airtel hatuwezi kuendelea bila kuwepo watu wanaotumia huduma zetu. Watu hawa ndio mtaji wa Kampuni,” amesema Gabriel.

Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengenti, John Wanyancha amesema kuwa kampuni hiyo imetoa lita 1,250 ya vitakasa mikono nyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na maambukiza ya virusi.

Mwenyekiti wa Rotary Club, Agnes Batenga amesema Rotary imetoa Sh. 250 milioni kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19).

“Shilingi milioni 183 zitatumika kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya maji safi ambavyo vitasambazwa katika vituo maalumu vya kuhudumia wagonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Amana, Zanzibar, Hospitali ya Mawenzi na Hospitali ya Mount Meru,” amesema Agnes.

Amesema Sh. 67 milioni zitatumika katika kutekeleza miradi ya kudhibiti ugonjwa wa Corona nchini kupitia Club za Rotary.

error: Content is protected !!