Wednesday , 1 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif amuunga mkono Lissu, Membe na Zitto wasema…
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif amuunga mkono Lissu, Membe na Zitto wasema…

Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo
Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetangaza kumuunga mkono Tundu Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Msimamo huo umetolewa jana Jumatatu tarehe 21 Septemba 2020 na Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo katika mkutano wa kampeni za urais za chama hicho Zanzibar, zilizofanyika Jimbo la Donge.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Janeth Rithe, Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT-Wazalendo, Maalim Seif ameutumia mkutano huo wa kampeni kumuidhinisha Lissu kuwa mgombea wao wa urais badala ya Bernard Membe, aliyepitishwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.

“Saa chache zilizopita, katika mkutano wake wa kampeni kwenye Jimbo la Donge, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif amemuidhinisha Tundu Lissu kuwa mgombea kwa wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inaeleza taarifa ya Rithe.

Hata hivyo, Membe amepinga msimamo huo, akisema kwamba yeye ndiye mgombea Urais wa Tanzania wa ACT-Wazalendo, aliyekabidhiwa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Membe ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter, huku akisisitiza kwamba, taarifa zinazotolewa kwamba ACT-Wazalendo imeungana na Chadema kwenye mbio za urais si za kweli.

Maalim Seif ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar akizungumza katika mkutano huo, alisema kwa vyovyote itakavyokuwa anajua Rais wa Tanzania ni Lissu.

Benard Membe (kulia) akiwa na Maalim Seif

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumzia wagombea ubunge na udiwani wa ACT-Wazalendo walioenguliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Alisema kama Lissu akitawadhwa kuwa Rais wa Tanzania, atamwambia amrejeshee wagombea wake na ikitokea Rais John Magufuli amechaguliwa tena kushika wadhifa huo, pia atamwambia vivyo hivyo.

“Ndugu zangu tuombe tujaaliwe nipate Serikali, nikishapata serikali vyovyote itavyokuwa, mimi najua Jamhuri ya  Muungano Rais atakua Tundu Lissu, maana Tundu Lissu ni rahisi kumwambia nirejeshee watu wangu,” alisema Maalim Seif.

“Lakini hata kwa bahati mbaya apite Magufuli, nachukua ndege naenda hadi Ikulu nasema nataka watu wangu warejeshwe,” alisema

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, Membe ambaye ni Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, alitumia akaunti yake ya Twitter kuzungumzia hilo.

“Mimi ndiyo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT- Wazalendo.”

“Mimi ndiye niliyekabidhiwa Ilani ya Chama hicho kuinadi kote nchini kwenye uchaguzi huu. Taarifa zinazosambaa kuwa tayari tumejiunga na Chadema katika ngazi ya Urais siyo za kweli,” aliansika Membe, aliyejiunga na ACT-Wazalendo tarehe 7 Julai 2020 akitokea CCM alikofukuzwa.

Membe aliwahi kunukuliwa akisema, atakuwa tayari kumuunga mkono mgombea yeyote wa upinzani mwenye nguvu kati yake au hata Lissu ili kuing’oa CCM madarakani.

Kauli hiyo, imekuwa ikizungumzwa pia na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kwamba majadiliano baina ya chama anachokiongoza na Chadema yanaendelea ikiwemo kuachiana nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Zitto alisema, ushirikiano wa vyama hivyo na kusimamisha mgombea mmoja ndiyo matamanio yao na ya Watanzania kuliko kuingia katika uchaguzi bila kushirikiana.

Zitto ambaye ni mgombea Ubunge Kigoma Mjini leo Jumanne ameandika kwenye akaunti yake Twitter akisema “Nimezunguka nchi yetu na kuona hisia za Watanzania. Juzi Mtwara Mjini alinifuata mama mtu mzima sana na kuniambia “mwanangu mmeshindwa kukubaliana Mgombea mmoja? Tafadhali mwanangu jitahidini.”

“Nilipata uchungu sana moyoni. Watanzania wanataka mabadiliko. Tutawapa,” amesema Zitto

Kauli za Zitto zinafanana na zilizowahi kutolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwamba watakuwa tayari kushirikiana na vyama vyovyote makini kwenye uchaguzi huo.

Mbowe aliwataka wanachama na wagombea wa Chadema kuwa tayari kupokea maamuzi wa hayo hasa suala la kuachiana udiwani na ubunge kwenye maeneo ambayo wanaona mgombea wa chama fulani anakubarika.

Hivi karibuni, Lissu akiwa Visiwani Zanzibar, alitangaza Chadema kumuunga mkono, Maalim Seif kwenye nafasi ya urais akisema, yeye na chama chake hawawezi kupinga harakati za muda mrefu za mwanasiasa huyo visiwani humo.

Kwa muda mrefu chama cha Chadema na ACT-Wazalendo vilitangaza kuwa katika meza ya majadiliano juu ya ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, licha ya kwamba hadi sasa vyama hivyo havijaweka wazi maazimio ya majadiliano hayo.

Hata hivyo, mara kadhaa viongozi wa vyama hivyo vya upinzani wamenukulowa na vyombo vya habari wakionesha dhamira ya kuungana katika uchaguzi huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!