May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zitto: Hamumkomoi Mbowe, Rais Samia usiingie kwenye mtego

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

KIONGOZI wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi, aliyofunguliwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na wenzake watatu, hayamkomoi kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani Tanzania.Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Zitto ametoa kauli hiyo leo Jumapili, tarehe 8 Agosti 2021, akielezea tathimini ya hali ya kisiasa Tanzania, kwenye kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, kilichofanyika visiwani Zanzibar.

Mbowe na wenzake, Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohammes Abdillah Lingwenya, wanakabiliwa na mashtama hayo katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 63/2020, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Kwa sasa mwanasiasa huyo na wenzake wako mahabusu ya Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, hatua ya Mbowe kufunguliwa kesi hiyo hairudishi nyuma harakati za vyama vya siasa vya upinzani kuipigania Tanzania, bali inalirudisha nyuma kimaendeleo Taifa hilo.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo

“Hawamkomoi Mbowe, wala hawatuvunji moyo wa kupambania Tanzania yenye usawa wa kisiasa na kuheshimu utofauti wetu wa mawazo. Wanalichelewesha tu Taifa letu kupata umoja na maendeleo ya kiuchumi. Wanataka turudi kule kule, ambapo hatupaswi kurudi,” amesema Zitto.

Mwanasiasa huyo amedai kuwa, kesi ya inayomkabili  Mbowe na wenzake ni mtego kwa Rais Samia, uliowekwa na baadhi ya watu wanaotaka kuirudisha Tanzania gizani.

“Nimwombe sana Rais Samia asikubali na asiingie kwenye mtego wa kuendeshwa na watu wanaotaka kuturudisha tulipotoka, watu anaotaka turudi gizani. Aidha, ni vema hawa wanaotaka turudi gizani, wampe nafasi rais atupe uongozi na maono yake badala ya kuendelea kuishi ndoto zao za miaka ambayo haitarudi tena kwa uwezo wake Mola wetu,” amesema  Zitto.

Zitto amemuangukia Rais Samia akisema “wito wangu na Viongozi wenzangu kwa  rais, ni kuingilia kati na kumaliza jambo hili la kisiasa kwa njia za kisiasa. Tunao uzoefu wa namna baadhi ya watendaji wanavyotumiwa kisiasa kutumia kesi kama fimbo kwa viongozi wa kisiasa wa Upinzani.”

error: Content is protected !!