Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Zanzibar tuko tayari njooni kuwekeza-Rais Mwinyi
Habari za Siasa

Zanzibar tuko tayari njooni kuwekeza-Rais Mwinyi

Spread the love

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kufungua milango kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje, ili kukuza diplomasia ya uchumi na kufanikisha maendeleo ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

 Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, huko katika Hoteli ya Golden Tulip nje kidogo ya mji wa Zanzibar, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji, kati ya Italia na Zanzibar.

Amesema milango ya Zanzibar iko wazi, salama, na ipo tayari kwaajili ya biashara na uwekezaji, hasa kwa kuzingatia kwamba Zanzibar ni nchi yenye vivutio vingi vikiwemo vya utalii na mandhari tulivu ya kupendeza, pamoja na maeneo maalum yaliyotengwa ili kutekeleza azma hiyo.

Ameeleza kuwa ili kufanikisha hayo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa mazingira bora ya uwekezaji, yakiwemo sera mahsusi za kuwavuta na kuwawezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, kutekeleza dhamira ya kuwekeza hapa nchini.

“Kwa mfululizo tumekuwa tukipitia na kuimarisha sera zetu za uchumi wa darala la juu na wa kima cha chini, ili kuweza kukidhi mahitaji na matarajio ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini kwetu, na hata kwa wananchi wetu wenye azma ya kuwekeza,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha ameukaribisha ujumbe wa Wakala wa Biashara kutoka Italia (Italy Trade Agency) kuongeza kiwango cha miradi ya uwekezaji, Zanzibar hapa na Tanzania kwa ujumla, akisema kuwa nchi mbili hizi zimejenga mahusiano ya diplomasia ya uchumi kwa miaka mingi.

Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa, fungamano la kibiashara na kiuchumi kati ya Zanzibar na Italia ambalo ni la kihistoria, linathibitishwa na idadi kubwa ya Miradi ya Wawekezaji wa nchi hiyo Zanzibar, kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo kwa sasa imefikia 84, ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani 603. 61 inayotoa fursa za ajira takriban 5,721.

Amesema katika kuhamasisha dhamira hiyo Serikali itahakikisha inayafanyia kazi mapendekezo yote muhimu kupitia Kongamano hilo, ili kutoa fursa ya kukuza ushirikiano, kwa maslahi ya maendeleo ya kiuchumi baina ya nchi mbili hizo, na “kwa mikono miwili, waje kuwekeza katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za Uvuvi, Mazingira, Viwanda na Uchumi wa Buluu.”

Kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, amepongeza dhamira ya wawekezaji kutoka Italia kufukuzia nafasi za kuwekeza zaidi visiwani Unguja na Pemba, hatua ambayo inaifungulia Zanzibar fursa za kujiletea maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharif Ali Sharif, amesema Italia inashika nafasi ya tatu katika uwekezaji Zanzibar na anaamini kongamano hilo la pili katika mnasaba huo, litafungua njia nyingi zaidi za kukuza ushirikiano baina ya pande hizo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCCIA), Ali Suleiman Amour, ameeleza matumaini yake kuwa mjumuiko wa wadau mbalimbali wa ndani ya serikali na sekta binafsi wakiwemo wafanyabiashara wa Kitaliano utachagiza ukuaji wa uchumi kutokana na shughuli za uwekezaji. Anaamini ushirikiano huo ni daraja la kufanikisha mipango ya kuinua uchumi wa Zanzibar huku akitilia maanani utayari wa serikali na taasisi zake kutatua vikwazo vinavyozorotesha kasi ya ujenzi wa mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta tofauti zinazolenga kukuza uchumi.

Balozi wa Italia nchini Tanzania, Marco Lombardi, ameishukuru Serikali ya Zanzibar na wawekezaji wote kwa namna walivyoitika mualiko wa kushiriki kongamano hilo; akitarajia ishirikiano zaidi kwa kila mhusika kwa lengo la kuisaidia nchi kuimarisha uchumi wake na ustawi wa wananchi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!