Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Waziri Mbarawa atoa ripoti ajali ya ndege hadharani, “mhudumu ndiye aliyefungua mlango”
Habari za SiasaTangulizi

Waziri Mbarawa atoa ripoti ajali ya ndege hadharani, “mhudumu ndiye aliyefungua mlango”

Ndege ya Precision ikiwa imezama katika ziwa Victoria baada ya kushindwa kutua uwanja wa Ndege wa Bukoba, Kagera
Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetoa taarifa rasmi kuhusu ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air, ikisema ilitumbukia ziwani baada ya Hali ya hewa kubadilika ghafla. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akitoa taarifa hiyo ya awali kwa umma, leo tarehe 24 Novemba, 2022 Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema rubani wa ndege hiyo, alizunguka angani kwa muda wa dakika 20 akitarajia hali ya hewa kubadilika, lakini haikubadilika kitendo kilichopelekea kutafuta njia ya kuruka.

“Kuna baadhi ya masuala yamejitokeza katika ripoti ya awali, la kwanza hali ya hewa ripoti inasema ilirupitiwa kuwa nzuri mpaka saa 2 asubuhi ambapo ilibadilika ghafla na mvua kuanza kunyesha ikiambatana na radi. Ndege iliingia anga ya Bukoba saa 2.45 na kukuta hali ya hewa imebadilika,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema “ndege ilizunguka takribani dakika 20 ikitarajia uwezekano wa hali ya hewa kubadilika, baadae rubani aliamua kutafuta njia ya kuruka. Kutokana na maelezo ya abiria walionusurika, njia ya ndege ilikuwa inaonekana. Walieleza waliona njia ya kuruka na kitua ndege kabla ndege kugonga kwenye maji.”

Waziri huyo wa uchukuzi amesema kuwa, ripoti hiyo inaonesha kuwa Uwanja wa Ndege wa Bukoba uko katika hali nzuri, ukiwa na kituo cha kuzima moto na kikosi chenye watu 10 wenye jukumu la uokoaji.

Akielezea namna zoezi la uokoaji lilivyofanyika, Prof. Mbarawa amesema ripoti inaonyesha mlango wa ndege ulifunguliwa na mhudumu wa ndege kwa msaada wa abiria pamoja na wavuvi waliokuwa nje.

“Kuhusu namna mlango ulivyofunguliwa, ni kweli ulifunguliwa na mhudumu wa ndege kwa msaada wa abiria hata hivyo, hiyo ripoti ya uchunguzi ilivyosema wananchi waliokuwa wanafanya uvuvi karibu na ajali walifika dakika tano baada ya ajali kutokea na kuanza kufungua mlango, hali hiyo ilimpa ujasiri mhudumu wa ndege kufungua mlango,” amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amesema majina ya wavuvi na mtumishi wa ndege walioshiriki zoezi la kufungua mlango, yatatajwa baada ya uchunguzi huo kukamilika na ripoti kutolewa.

Akizungumzia mjadala wa vyombo vya uokozi kuchelewa kufika eneo la tukio kutoa msaada, Prof. Mbawara amesema “katika ajali za majini tunaongozwa na mkataba wa kimataifa wa kuhudumia masuala ya utafutaji na uokozi majini wa 1974 ambao nchi tumeridhia.”

“Mkataba umetoa mwongozo pale inapotokea ajali katika maji, inamtaka mtu au kikundi walioko karibu na eneo la ajali kuwajibika katika uokozi na kutoa taarifa kwa vyombo vya uokozi na kwa mamlaka husika. Watu hao wataendelea kuwajibika. Ni kawaida watu waliokaribu kusaidia kuokoa… walishiriki zoezi, walitimiza wajibu wao wa kizalendo na waliwajibikia Taifa,” amesema Prof. Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa

“Kuhusu kuchelewa kufika boti ya uokozi nitoe ufafanuzi tunayo boti ya uokozi Ziwa Victoria wakati ajali inatokea boti ilikuwa katika doria kwenye eneo mbali na uwanja wa ndege wa Bukoba ikiwa katika kutekeleza majukumu yake.

“Kutokana na umbali huo boti ilipofika kwenye ajali shughuli za uokoaji zilikuwa zimekamilika. Naomba kusisitiza kuwa ajali hii haikutarajiwa na ajali inapotokea kila mtu ana wajibu wa kushirikiana,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbawara amesema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea kufanywa na wataalamu wa masuala ya ndege kutoka nchini, Ufaransa na Uingereza.

Amesema ripoti nyingine ya awali itatolewa ndani ya siku 30 na ripoti ya mwisho itatolewa ndani ya miezi 12 baada ya ajali kutokea.

“Zoezi la uchunguzi wa kina ajili ya kuandaa taarifa ya awali ya ajali ya ndege unaendelea,” amesema Prof. Mbarawa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!