WATU wawili wamefariki duniani na wengine sita kuokolewa wakiwa hai baada ya duara walilokuwa wakichimba madini ya dhahabu kutitia katika Mgodi wa Wachapakazi uliopo Kijiji cha Nyandolwa wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga. Anaripoti Paul Kayanda – Shinyanga. (endelea…)
Miili ya watu hao iliokolewa kwa nyakati tofauti katika zoezi la uokoaji lililodumu kwa muda wa siku 14 kuanzia tarehe 15 Septemba hadi 1 Oktoba mwaka huu ambapo mwili wa pili ulipatikana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mmoja kati ya wakurugenzi wa mgodi huo, Joseph Makoba amesema baada ya ajali hiyo kutokea na kufanya uokoaji, walibaini watu wawili wamesalia.
“Huwa tuna takwimu za watu wanainga shimoni kufanya kazi. Takwimu zilionesha wamebaki wawili hivyo tulianza kuwatafuta kama binadamu wenzetu na nguvu kazi.
“Baada ya siku nne kupitas tulifanikiwa kupata mwili wa kijan a mmoja ambaye ni mkazi wa Nyang’wale kisha siku iliyofuata tukampata wa mwisho ambaye alikuwa mkazi wa Segese. Wote tayari tumewasitiri kwenye nyumba zao za milele.
“Suala la msingi kwetu ni usalama kwanza lakini hizi ni ajali kama ajali nyingine hivyo tunaendelea kuzidisha juhudi kuhakikisha usalama unazidi kuimarishwa ndani ya mgodi,” amesema.
Aidha, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Jastine Siyaraha ameuomba uongozi wa mgodi huo kuimarisha suala la usalama mgodini ili yasitokee matukio ya aina hiyo mara kwa mara.
“Mimi ni mfanyakazi wa mgodi huu, tangu ajali itokee mgodi umefungwa, hivyo tumeathirika sana kiuchumi hasa ikizingatiwa tunategemea shughuli za uchimbaji wa madini kuendesha maisha yetu,” amesema.
Leave a comment