MWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Stephen Wasira amesema mikutano ya hadhara ikianza kufanyika itakiamsha Chama kilichoko madarakani cha CCM, ili kitimize mambo iliyoahidi kwa wananchi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Wasira ameyasema hayo leo Alhamisi, katika mkutano wa mtandaoni ulioendeshwa na taasisi ya Watch Tanzania, baada ya kuulizwa iwapo CCM itaathirika na ruksa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Wasira aliyekuwa Mbunge wa Bunda kwa tiketi ya CCM, amesema kitendo cha vyama vya siasa vya upinzani kuruhusiwa kufanya mikutano hiyo, hakitaathiri chama chake.
“Sisi tunasema kama wasimamizi wa ilani kuna faida hakuna hasara yoyote sababu ni chama cha siasa tuemaminiwa na tumeshika dola, tunaendesha Serikali lakini kuna ahadi tumewapa Watanzania katika ilani. Kuruhusu mikutano ya hadhara wanatuamsha zaidi tusilale ili tutimize tulichoahidi lakini tukitetee zaidi,” amesema Wasira.
Aidha, Wasira amevitaka vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu kwa kuwa siasa za fujo ndiyo ilikuwa sababu ya Hayati John Magufuli, kupiga marufuku mikutano ya hadhara.
Katika hatua nyingine, Wasira amesema Rais Samia anatembea katika maneno yake, kwa kufanya vitu ambavyo aliviahidi ikiwemo kukuza demokrasia na kutoa uhuru kwa vyombo vya habari.
Leave a comment