KAMATI Tendaji ya Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), tarehe 18 Mei 2021, itafanya uchaguzi kujaza nafasi za viongozi wa baraza hilo, waliofukuzwa uanachama Novemba 2020, kwa tuhuma za usaliti. Anripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa ya uchaguzi huo imetolewa leo Jumamosi tarehe 15 Mei 2021, na Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara, Benson Kigaila.
“Kamati tendaji ya Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) itakutana Jijini Mwanza tarehe 18 Mei 2021, kwaajili ya kufanya uchaguzi wa viongozi hao kwa mujibu wa muongozo wa baraza hilo kifungu cha 7.8.5 (a)(b)(c)(d),”imesema taarifa ya Kigaila.
Nafasi za Viongozi wa BAWACHA zitakazojazwa na Kamati yake Tendaji ni, Ukatibu Mkuu, iliyokuwa inaongozwa na Grace Tendega, kabla hajafukuzwa Chadema.
Nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu Bara, iliyokuwa chini ya Jesca Kishoa pamoja na Katibu Mwenezi, iliyokuwa imeshikwa na Agnesta Lambart.
Taarifa ya Kigaila imewataja wanachama wa Chadema walioteuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho, kugombea nafasi hizo.
“Kamati kuu ya chama iliyokutana kidigitali tarehe 12 Mei 2021, kwa mujibu wa kanuni za chama kifungu cha 7.2.6 pamoja na mambo mengine, ilifanya usaili, kujadili na kuteua wagombea wa nafasi mbali mbali zinazotarajiwa kufanyiwa uchaguzi katika BAWACHA,” imesema taarifa ya Bawacha.
Nafasi ya Ukatibu Mkuu BAWACHA, walioteuliwa kugimbea ni Asia Daud Msangi, Catherine Nyakao Ruge na Esther Cyprian Daffi.
Wakati Brenda Rupia Jonas, Emma Theobald Boki na Nuru Elias Ndosi, wakiteuliwa kugombea Unaibu Katibu Mkuu wa baraza hilo Bara, huku nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu BAWACHA akiteuliwa Bahati Chum Haji, kugombea.

Kwa upande wa Katibu Mwenezi Bawacha, walioteuliwa kugombea ni, Aisha Machano Ame, Husna Amri said na Sigrada Wilhem Mligo.
Nje ya Tendega na wenzake, viongozi wengine wa BAWACHA waliofukuzwa ni Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza hilo Taifa na Hawa Mwaifunga (Makanu Mwenyekiti BAWACHA Zanzibar).
Leave a comment