SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, ameanza kutimiza ahadi yake ya kuteua wapinzani serikalini, baada ya kumteua Queen Cuthbert Sendiga, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar Es Salaam…(endelea).
Rais Samia amefanya uteuzi huo leo Jumamosi tarehe 15 Mei 2021, na kutangazwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa.
Sendiga anachukua nafasi ya Ali Hapi, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
“Rais Samia amemteua Queen Cuthbert Sendiga, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Sendiga anachukua nafasi ya Ali Salum Hapi, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora,” imesema taarifa ya Msigwa.
Sendiga alikuwa Mgombea Urais wa Tanzania, katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, kupitia chama cha ADC.
Hatua hiyo ya Rais Samia kumteua Sendiga kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, inatimiza ahadi yake aliyoitoa katika mkutano wake na Wazee wa Dar Es Salaam, kwamba katika Serikali yake atashirikisha wapinzani, ili kuleta Umoja wa Kitaifa.

Rais Samia amefuata nyayo za mtangulizi wake, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, za kuteua viongozi wa Serikali kutoka vyama vya upinzani.
2017, Dk. Magufuli alimteua aliyekuwa Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro.
Mghwira ameuongoza mkoa huo kuanzia mwaka 2017 hadi 2021, baada ya kustaafu.
Rais Samia amemteua aliyekuwa Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, kurithi mikoba ya Mghwira Kilimanjaro.
Leave a comment