Wednesday , 1 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wapiga kura 216,282 kupiga kura uchaguzi mdogo Mbarali, kata sita  
Habari za SiasaTangulizi

Wapiga kura 216,282 kupiga kura uchaguzi mdogo Mbarali, kata sita  

Spread the love

Wapiga kura 216,282 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kupiga kura kesho tarehe 19 Septemba 2023 kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara. Anaripoti Matilda Peter, Dar es Salaam…(endelea).

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya leo tarehe 18 Septemba 2023 wakati akisoma risala kwa ajili ya uchaguzi huo na kuongeza kwamba uchaguzi utahusisha vituo 580 vya kupigia kura.

“Katika uchaguzi huu kuna jumla ya wapiga kura 216,282 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao watashiriki kuchagua viongozi wao.  Aidha, uchaguzi huu utahusisha vituo 580 vya kupigia kura vilivyobainishwa,” amesema Jaji Mwambegele.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele

Kata zenye uchaguzi ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo na Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba.

Mwenyekiti wa Tume amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala wa vyama, wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba hawapigi kampeni siku ya kupiga kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

“Alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi haviruhusiwi kutumika kesho tarehe 19 Septemba, 2023 ambayo ni siku ya uchaguzi,” amesema.

Jaji Mwambegele ameongeza kwamba zoezi la kupiga kura katika maeneo yote ya uchaguzi litafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Ameongeza kwamba vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.

“Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni katika mstari na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni,” amesema.

Jaji Mwambengele amebainisha kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye   Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye kata husika na wana kadi zao za mpiga kura.

Ameongeza kuwa, hata hivyo, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala.

“Mojawapo ya kitambulisho mbadala ambacho mpiga kura anaweza kutumia ni Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” amesema.

Mwenyeki wa Tume amesisitiza kwamba ili mpiga kura aruhusiwe kutumia kitambulisho mbadala ni sharti awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura katika kituo anachokwenda kupiga kura.

“Katika kituo cha kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na watoto kituoni,” amesema.

Kuhusu wapiga kura kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, Jaji Mwambegele amesema hilo ni sharti la kisheria na kwamba maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na kuridhiwa na vyama vyote vya siasa, Serikali na Tume yanaelekeza hivyo.

Alisisitiza kwa kusema “wapiga kura watatakiwa kuondoka kituoni mara wanapomaliza kupiga kura ili kuepusha msongamano na vitendo vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani.  Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura”.

Ametoa rai kwa wapiga kura katika Jimbo la Mbarali na kata sita zinazohusika na uchaguzi huu mdogo, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.

Jumla ya vyama 17 vya siasa vinashiriki kwenye uchaguzi huo mdogo, vyama hivyo vinajumuisha AAFP, ACT–WAZALENDO, ADA–TADEA, ADC, CCK, CCM, CUF, Demokrasia Makini, DP, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD, UPDP na NCCR–MAGEUZI.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

error: Content is protected !!