MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Selukamba ametoa siku saba kwa halmashauri ya Iramba, Mkarama, Singida Dc na Manispaa kuhakikisha miradi ya elimu ya sekondari (Sequip) inakamilika na kukabidhiwa ifikapo tarehe 25 Septemba mwaka huu. Anaripoti Danson Kaijage, Singida (endelea).
Ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Septemba 2023 kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa miradi hiyo ambayo inasimamiwa na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri husika.
Amesema mkandarasi ambaye anachelewesha kazi wakati vifaa vyote vipo anatakiwa kupunguziwa kazi na kupewa mtu mwingine ambaye anaonesha kuwa na juhudi za kufanya kazi.
Katia hatua nyingine amewaonya wakandarasi ambao watachezea fedha za serikali kwa kutekeleza miradi chini ya kiwango na kusema kuwa wakandarasi hao hawatavumiliwa wala kufumbiwa macho na badala yake hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Lazima tutambue kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo hivyo hakuna atakaye kubali kuona fedha zinachezewa,” amesema.
Ziara ya mkuu wa Mkoa wa Singida ya kukagua miradi inaendelea leo ikiwa ni kuhakiki miradi inayotekelezwa katika mkoa huo inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.
Leave a comment