May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waitara atumwa kuinadi CCM Buyungu

Spread the love

ALIYEKUWA mbunge wa Ukonga, kupitia Chama cha Demokrasia (CHADEMA), Mwita Mwaikabe Waitara, anaelekea jimboni Buyungu, wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, kukiongezea nguvu chama chake kipya (CCM). Anaripoti Yusuph Katimba…(endelea).

Waitara aliyetangaza kujiengua Chadema jana Jumamosi na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, anatarajiwa kutua Kakonko, muda wote kuanzia kesho Jumatatu.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya CCM na zilizothibitishwa na Waitara mwenyewe zinasema, mwanasiasa huyo amesafiri leo asubuhi kwa ndege kuelekea Mwanza; tayari kujiunga na timu ya kampeni ya chama hicho iliyoko mkoani Kigoma.

Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Buyungu, unafanyika kufuatia kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mwalimu Samson Kasuku Bilago (Chadema).

Mwalimu Bilago (54), alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Mei mwaka huu.

Alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kuota kinyama sehemu ya haja kubwa unaofahamika kwa jina la hemorrhoids au piles – (bawasiri).

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kuwa uchaguzi huo katika jimbo hilo utafanyika tarehe 12 Agosti.

Katika uchaguzi huu, ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya Mhandisi Christopher Chiza (CCM) na Elias Kanjero (Chadema).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online jana – Jumamosi – majira ya saa tatu usiku, Waitara alisema, “…mi kweli nimepanga kwenda Mwanza kwa shughuli zangu binafsi na baadaye nitakwenda kwenye kampeni Buyungu.”

Alisema, “ninakwenda Buyungu kukinadi chama changu na kuhakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi huu. Ninakwenda Buyungu kueleza wananchi madhaifu ya Chadema na ambayo yamenisababishia mimi kuondoka.

“Ninakwenda Buyungu kueleza ukweli ambao baadhi ya wabunge na viongozi wakuu wa chama hicho, hawataki au wanaogopa kuusema.”

Akizungumzia kuondoka kwake ghafla Chadema na kujiunga na CCM, Waitara alisema, “nimeshindwa kuvumilia hila na ghiliba za Mbowe (Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa chama hicho) na genge lake.”

Anasema, “hawa watu wamekuja Ukonga kuja kuvuruga Chadema. Mbowe na watu wake wamekuja Ukonga kwa ajili ya kuweka mtandao wao wa kuhakikisha anashinda uchaguzi mkuu ndani ya chama. Wamekuja Ukonga kunishughulikia.

“Hivyo basi, nimeona ni vema nikaondoka ili niweza kutimiza malengo yangu ya kuwatumikia wananchi wa Ukonga walionichagua kwa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.”

Waitara anadai kuwa ndani ya Chadema kuna matatizo makubwa yanayosababishwa na Mbowe kutaka kukigeuza chama hicho kuwa kampuni yake binafsi.

“Haya siyo maoni yangu binafsi. Wapo watu wengi ndani ya chama hicho wanaofikiri kama mimi, ingawa wao wameamua kubaki kuendeleza mapambano ndani,” ameeleza.

Waitara alitangaza kuondoka Chadema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na kuongeza, “nimeamua kuondoka kwa kuwa ndani ya Chadema hakuna demokrasia.”

Alipokelewa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Kabla ya kujiunga na Chadema, Waitara aliwahi kuwa katibu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), mkoani Tanga.

Alikuwa mmoja wa “wapinzani” wakuu wa Mbowe, kuendelea kugombea uenyekiti wa chama hicho, katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

error: Content is protected !!