October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wabunge wailipua LATRA kwa kushindwa kusimamia Ubber, Bolt

Spread the love

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Sheria ndogo, Jasson Rweikiza amesema baadhi ya kanuni za sheria ndogo zilizotungwa na kutumiwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika usimamizi wa kampuni za teksi mtandaoni, zinachafua taswira ya Bunge na kukwamisha maisha ya Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Ametolea mfano kuwa kanuni hizo zilisababisha  kampuni za teksi mtandao – Ubber na Bolt kusitisha huduma za usafiri wa magari nchini licha ya kwamba zilikuwa zinatoa huduma nzuri na za gharama nafuu kwa wananchi.

Mbunge wa Viti Maalum, Judith Kapinga,

Kampuni ya Bolt na Ubber, zilisitisha huduma zake hivi karibuni, baada ya LATRA kuanzisha kanuni za usimamizi ambazo zilianzisha kiwango cha ukomo cha kamisheni cha asilimia 15 ambazo kampuni hizo zinawatoza madereva wake. Awali, kampuni hizo zilikuwa zinatoza kati ya asilimia 20 hadi 25.

Rweikiza ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Septemba, 2022 wakati akihitimisha mjadala wa taarifa ya kamati ya sheria ndogo kuhusu uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa bungeni kwenye mkutano wa sita na wa saba.

Amesema sheria ndogo hazina lengo hilo la kukwamisha maendeleo kwa watanzania hivyo, wale wanaotunga sheria hizo wajitahidi kuzingatia sheria mama, kuwa na utu na kupenda maendeleo.

“Sheria zinachafua taswira ya bunge, mfano Bolt na Ubber zimefunga kabisa biashara zao ambao zilikuwa ni huduma nzuri, zina gharama nafuu kwa mwananchi, unapiga simu dakika mbili tu umepata usafiri, sasa hivi zimesimama kabisa.

“Hii sio kuboresha masilahi ya watanzania au ufanisi wa maisha kuwa mazuri ni kukwamisha. Sheria ndogo hazina lengo hilo, wale wanaotunga sheria wajitahidi kuzingatia sheria mama, kuwa na utu, kupenda maendeleo na si kukwamisha maendeleo.

Awali Mbunge wa Viti Maalum, Judith Kapinga (CCM) ameshauri LATRA, isisimamie kampuni za mifumo ya teksi mtandaoni, ikiwemo za Bolt na Ubber, akidai siyo kampuni za usafirishaji, bali ni za ubunifu.

“LATRA hawakuwa na mamlaka ya kutunga kanuni zile ambazo zinasababisha kampuni za ubunifu na teknolojia kusitisha biashara zao. LATRA inahusiana na kuratibu usafiri na sio masuala ya teknolojia. Bolt na Ubber sio kampuni za usafirishajim ni kampuni za ubunifu na teknolojia,” amesema Kapinga.

Mkurugenzii LATRA, Habibu J. Suluo

Mbunge huyo viti maalum amesema, kitendo cha kampuni hizo kusitisha huduma, kumepelekea madereva wake kukosa ajira pamoja na wananchi kukosa usafiri wa bei nafuu.

“Wale waliokuwa wanawatetea hawafanyi baishara, wananchi wamekuwa wanapata ahueni wenyewe mambo yao ni magumu. Nia yetu mwananchi maisha yake kurahisishika kama kulikuwa kuna jambo si wanakaa mezani tunalitatua. Kwa hiyo iliangalia upande mmoja, wa wananchi ambao maisha yao yamerahisishwa haukuangaliwa,” amesema Kapinga.

Kapinga ameishauri kanuni zilizotungwa na LATRA dhidi ya kampuni hizo zirekebishwe, kwa kuwa zilitungwa pasina kuwashirikisha wamiliki wake.

“Ningependa niishauri Serikali yangu wawashauri LATRA, kanuni hizi wazivute nyuma. Kwa kweli ni kanuni ambazo hazina maslahi kwa madereva wala wananchi ambao walikuwa wananufaika kwa huduma ya Bolt na Ubber,” amesema Kapinga na kuongeza:

“Kanuni hizi zilitungwa kwa kuangalia juu juu, sio kwa kufanya utafiti wa kina na kuhakikisha kwamba tunalinda makundi yote. Hawa Bolt na Ubber hizi sio teknolojia zao, hapa Tanzania wananunua hati miliki kwa hiyo wenyewe wanazilipia, walipaswa kusikilizwa kwenye kamisheni wanayopata, asilimia ngapi ni faida zao binafsi.”

Hayo yamejiri ikiwa ni wiki chache zimepita tangu LATRA iziite mezani kampuni hizo za teksi mtandao, kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali zilizopelekea wasitishe huduma zao lakini hadi sasa hakuna kampuni iliyobatilisha uamuzi wake.

error: Content is protected !!