October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Zungu; Baada ya kupendekeza tozo miamala, ageukia intaneti

Spread the love

BAADA ya kufanikiwa kuishawishi Serikali kwa hoja yake ya kutaka kuwepo kwa tozo za miamala ili kuongeza mapato, Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu amegeukia intaneti na kusema Serikali inapoteza mapato katika eneo hilo. Anaripoti Apaikunda Mosha, TUDARco…(endelea).

Zungu ametoa maoni hayo leo tarehe 21 Septemba, 2022 bungeni jijini Dodoma mara baada ya kukamilika kwa kipindi cha maswali na majibu ambapo amemtaka Waziri wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari, Nape Nnauye kwenda kutazama eneo hilo.

Itakumbukwa  Zungu ndiye aliyekuja na wazo la Serikali kuweka tozo za miamala ya simu na tozo ya laini za simu wakati akichangia katika vikao vya Bunge, ambapo Serikai ilichukua wazo hilo na kulifanyia kazi. Hata hivyo wazo lake la tozo za laini ya simu liliachwa baada ya kuibua malalamiko mengi.

Zungu amesema Tanzania haina Pato la Ndani la Taifa (GDP) kwenye intaneti, na kwamba umiliki wa intaneti upo nje ya nchi na hivyo pesa zinakwenda nje ya nchi watanzania wanavyowasiliana kwa kutumia intaneti.

“Tunao service provides (watoa huduma) lakini na wao wanalipa hizi fedha nje ya nchi,” amesema.

“Sasa tunakuomba wewe Mheshimiwa Nape Nauye wewe ni mtaalamu na mwokozi wa nchi hii tunakutegemea wewe ufanye mabadiliko katika nchi yetu, tupate pesa nyingi kwenye intaneti, sasa hivi pesa nyingi sio kwenye voice call zipo kwenye data, nikuombe wewe  pamoja na wizara yako mshirikiane na wizara ya fedha mueke mkakati maalum kuhakikisha gate way ya intaneti inabaki nchini na mapato haya yabaki nchini tusilipe nje ya nchi,” amesisitiza Zungu.

Ameongeza kuwa  intaneti inaweza ikasambazwa maeneo mengi nchini na vijana wakawa watoa huduma.

“Najua jambo hili sio dogo litapigwa vita kwasababu ni suala la pesa hapa tunazungumzia national interest (maslahi ya Taifa) kusaidia Rais apate mapato na kusaidia vijana wapate ajira ya kuwa service providers (watoa huduma) kwenye intaneti.”

Akizungumzia hatua ya Serikali kupunguza na kuondoa baadhi ya tozo za miamala ya kielekroniki,Zungu amesema wananchi wengi wanalalamikia  kodi ya serikali lakini hawaangalii mapato yanayokatwa na mabenki na kampuni za simu.

“Lazima hii idhibitiwe, benki unatuma pesa wanachukua pesa nyingi kuliko serikali kwa asilimia kubwa sana lakini serikali inayojenga madarasa na vituo vya afya ndio inalaumiwa, kwahiyo kuna kitu kinachotengenezwa kuipiga serikali wakati pesa wanachukua watu wengine,” amesema na kuitaka Serikali kutazama namna ya kudhibiti benki na kampuni za simu kupunguza gharama zao.

“Niwaombe wananchi pamoja na wabunge unapotuma pesa tazama break down (mchanganuo) ya pesa inavoandikwa ili uweze kuona kiwango cha serikali kipo chini sana na mapato wanayochukua makampuni ya simu na taasisi za fedha yapo juu zaidi ya mapato wanayopata serikali,” amesema Zungu.

error: Content is protected !!