October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Viongozi CCM Rukwa watwangana makonde

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala, anadaiwa kumtwanga ngumi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) katika mkoa huo, Ramadhani Shabani baada ya kupishana kauli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Rukwa… (endelea)

Hayo yamejiri jana tarehe 20 Septemba, 2022 saa nane mchana kwenye ukumbi wa RRC Sumbawanga katika kikao cha kujadili majina ya wagombea nafasi ndani ya chama hicho.

Imeelezwa kuwa chanzo cha viongozi hao kutwangana ngumi ni kupishana kauli baada ya jina la mmoja wa wagombea wa nafasi ya uenezi Wilaya ya Sumbawanga vijijini, kukatwa.

“Chanzo kilikuwa ni kushutumiana kupokea rushwa na kurushiana maneno, ndiyo mwenyekiti wa mkoa akatoka jukwaa kuu na kumfuata huyo wa UVCCM wakaendelea kubishana na baadaye huyo wa mkoa akamtandika miguuni huyo wa UVCCM,” alieleza mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo na kuongeza kuwa;

“Desturi ya chama hicho, nafasi za uongozi huombwa kuanzia chini na kujadiliwa na vikao mbalimbali kabla ya uchaguzi wenyewe.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Rukwa, Ramadhan Shaban

Alisema kikao hicho kilikuwa kinajadili nafasi ya uenezi wa chama hicho Wilaya ya Sumbawanga vijijini ambapo awali Sekretarieti ya chama hicho ndani ya wilaya hiyo, ilipitisha majina matatu kugombea nafasi hiyo na yalivyofika kwenye Kamati ya Siasa wilaya, jina moja likakatwa.

“Sekretarieti ya Mkoa ilivyokaa, ilirudisha jina lililokatwa na mchakato ukaendelea kwenye Kamati ya siasa ya Mkoa ambayo ilipitisha majina kama yalivyoletwa na sekretarieti ya Mkoa.

“Halmashauri Kuu ya mkoa ilipokaa, jana (juzi) chini ya, Lukala ambaye ndiye pia alikuwa kiongozi kwenye kamati ya siasa mkoa, alionekana kutaka kuyageuka maamuzi yake ya awali.

“Hapo sasa ndipo shida ilipoanzia, watu wakawa wanahoji kwanini mwenyekiti anataka kula matapishi yake, ni kitu gani kimetokea,” alisema.

Alisema baada ya hali hiyo, shutma za kupeana rushwa zilizidi, ambapo upande mmoja ulikuwa unadai wanaotaka jina lisikatwe wamekula rushwa na upande mwingine unasema wanaotaka kukata jina wamekula rushwa za Sh 50,000.

Alisema katika hali hiyo, mwenyekiti wa UVCCM alisimama na kuhoji kwanini wajumbe waliopitisha majina kwenye Halmashauri ya Mkoa sasa wanataka kupindua maamuzi yao wenyewe.

Katika hali isiyo ya kawaida, inadawa mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa alishuka jukwaani na kumfuata mwenzake wa UVCCM na kuendeleza mabishano ambapo mwishoni alimrushia Makonde.

Hali hiyo ilifanya kikao hicho kuvunjika kwa muda na kurejea baadaye baada ya usuluhishi kufanywa.

“Tulivyorudi ndani, mwenyekiti wa mkoa alitaka huyo wa UVCCM atoke nje, yule kijana aligoma akisema yeye ni mjumbe halali wa hicho kikao na hawezi kutoka labda apewe barua rasmi,” kiliendelea kupasha chanzo chetu.

Baada ya mzozo huo, Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliamua Kamati ya Siasa Mkoa yote ipelekwe kwenye kamati ya maadili wachunguzwe juu ya tuhuma za rushwa walizotoleana.

Akizungumza na MwanaHalisi Online, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Rukwa, Ramadhan Shaban alikiri kupigwa ngumi na Mwenyekiti huyo.

Haya hivyo, alisema chama (CCM) kina utaratibu wake wa kushughulikia matatizo na kusisitiza kuwa jambo hilo ni siri.

“Siyo kwamba tulipigana bali mimi ndiye nilipigwa makonde na Mwenyekiti wangu sababu alitoka kwenye meza yake akanifuata, lakini pamoja na hayo, chama kina utaratibu wake wa kushughulikia mambo kama hana ndiyo sababu hata sisi viongozi tumeapa kulinda siri za chama ikijumuisha vikao.

“Hili lililotokea linabaki kuwa siri kwa kuwa lilitokea ndani ya chama chetu na taratibu zake za kushughulikia masuala kama haya, mimi kama kiongozi ni wajibu wangu kulinda siri za vikao japo naweza kusema kwamba hilo jambo lilitokea lipo,” alisema Shaban.

Aidha, MwanaHalisi ilizungumza na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Rainer Lukala kuhusu tuhuma hizo za na kudai kuwa hafahamu chochote.

Hata alipoelezwa kuwa Mwenyekiti wa  UVCCM amekiri kupigwa, Lukala alidai taarifa hizo ameziona katika mitandao ya kijamii na hajui zimeanzia wapi.

“Namimi naziona kwenye mitandao ya kijamii na sijui zimeanzia wapi na sijui hata aliyezisambaza analengo gani, ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho,” alisema Lukala.

error: Content is protected !!