UJENZI wa miradi ya maji katika Jimbo la Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara, umetajwa kuendelea kushika kasi, ambapo maji kutoka Ziwa Victoria yameanza kusambazwa kwa wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), unaendelea kutekeleza mradi wa maji ya bomba ya Chumwi-Mabuimerafuru.
Taarifa hiyo imesema kuwa, mradi huo unaogharimu fedha kiasi cha Sh. 1.7 bilioni, umepangwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Julai mwaka huu.
“Ujenzi unaoendelea kwa wakati huu ni, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 300,000 Kijijini Mabuimerafuru. Ujenzi wa vioski vya maji kwenye vijiji vya Chumwi na Mabuimerafuru.Mradi huu una thamani ya Tsh bilioni 1.7 na umepangwa kukamilishwa kabla ya tarehe 30.7.2023. Baadae, sehemu ya pili ya mradi huu ni ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji kwenye Vijiji vya Lyasembe na Murangi,” imesema taarifa hiyo.
Mbali na mradi huo, miradi mingine inayotarajiwa kuanza kutekelezwa jimboni humo ni pamoja na kuwasambaza maji ya bomba katika kata za Tegeruka (vijiji vitatu), Mugango (Vijiji vitatu), unaogharimu kiasi cha Sh. 4.75 bilioni.
Taarifa hiyo imesema kuwa, fedha za usambazaji maji hao zipo na kwamba utekelezaji wake utaanza Julai, 2023.
“Maji ya kata hizi mbili yatatoka kwenye bomba la maji la Mugango-Kiabakari-Butiama, ambalo limepangwa kukamilika kabla ya tarehe 30 Juni 2023.Usanifu wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba kwenye Kata za Busambara na Kiriba unakaribia kukamilika,” imesema taarifa hiyo na kuongeza.
“Kata hizi 2 zitasambaziwa maji kutoka kwenye tenki la mlima kong lenye ujazo wa lita 500,000. Maji ya tenki hili yatatolewa kwenye Bomba la Maji la Mugango-Kiabakari-Butiama.”
Leave a comment