October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Uamuzi kesi ndogo Mbowe, wenzake 19 Oktoba

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imeahirisha usikilizwa wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, hadi tarehe 19 Oktoba 2021, ikitarajia kutoa uamuzi wa kesi ndogo ya kesi hiyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo imeahirishwa leo Jumatano, tarehe 29 Septemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Mustapha Siyani, baada ya upande wa utetezi kuomba kufunga ushahidi na kuwasilisha mawasilisho yao ya mwisho dhidi ya kesi hiyo ndogo.

Akiahirisha usikilizwa wa kesi hiyo mdogo, Jaji Siyani amezitaka pande zote mbili kuwasilisha mawasilisho ya mwisho yasiyozidi kurasa tano, kwa njia za maandishi, Jumatatu tarehe 4 Oktoba 2021, kisha atatoa uamuzi tarehe 19 Oktoba mwaka huu.

“Shauri dogo limefika mwisho, mawakili mtaandaa hoja za maandishi kuisaidia mahakama kutoa uamuzi wa mwisho. Nitaandaa uamuzi wangu, tarehe 19 Oktoba 2021 itakuja kwa ajili ya uamuzi na kuendelea na usikilizwaji wa shauri,” amesema Jaji Siyani.

Upande wa utetezi umefunga ushahidi wao katika shauri hilo dogo la kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa yasitumike mahaiamani hapo kama ushahidi, ukidai yalichukuliwa kinyume cha sheria. Baada ya mke wa mshtakiwa huyo, Lilian Furaha Kibona, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Katika shauri hilo dogo, utetezi ulikuwa na mashahidi watatu, akiwemo Kasekwa na mkewe pamoja na mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya

Huku upande wa Jamhuri ukiwa na mashahidi watatu, ambao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Ramadhan Kingai, ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha. Detective Ricado Msemwa na aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Arusha, Mahita Omari Mahita.

error: Content is protected !!