Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tanzania, Burundi zakubaliana mambo 10
Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Burundi zakubaliana mambo 10

Spread the love

 

NCHI za Tanzania na Burundi, zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika mambo 10 muhimu ili kuimarisha uchumi wa pande zote mbili. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mambo hayo yameibanishwa leo Ijumaa, tarehe 22 Oktoba 2021 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye wakati wakitoa taarifa kwa umma kuhusu mazungumzo yao waliyofanya Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.

Jambo la kwanza ambalo nchi hizo mbili zitashirikiana, ni kuhusu ulinzi na usalama, ambapo Rais Samia amesema amekubaliana na Rais Ndayishimiye, kuimarisha ulinzi mipakani.

“Tulizungumza kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi na usalama na nilimhakikishia kuwa Tanzania itashirikiana na Burundi kulinda na kuimarisha ulinzi hususan katika mipaka,” amesema Rais Samia.

Naye Rais Ndayishimiye, amesema ushirikiano wa Burundi na Tanzania katika masuala ya usalama unaridhisha na kuomba ushirikiano huo uimarishwe zaidi hasa maeneo ya mipakani.

“Pamoja na hali tulivu uliopo, kuna kundi linaloongozwa na mwanasiasa wa Burundi, Alex Sinduhije, ambalo linashirikiana na kundi la kigaidi, lengo lake kubwa ni kuyumbisha usalama kwenye nchi za kanda za maziwa makuu, kinachosikitisha wanaangamiza maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia,’ amesema Rais Ndayishimiye.

Jambo la pili alilolitaja Rais Samia, ambalo wamekubaliana, ni ushirikiano katika sekta ya ujenzi kwa kuunganisha mtandao wa reli kati ya Tanzania na Burundi, kutoka Uvinza-Msongati-Gitega.

“Tumekubaliana kujenga reli ambapo kilomita 160 zipo upande wa Tanzania na kilomita 80 zipo upande wa Burundi. Nchi ya DR Congo ilionesha nia ya kujiunga na kuunganisha kipande cha reli kutoka Uvira Burundi hadi Kindu nchini humo,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, Januari 2021 nchi hizo tatu zilisaini hati ya makubaliano na ushirikiano kuhusu mradi huo utakaoziwezesha nchi hizo kusafirisha mizigo yao kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Jambo la tatu lililotajwa na Rais Samia ambalo walikubaliana kulifanyia kazi na Rais Ndayishimiye, ni Tanzania kuipatia Burundi maeneo ya kujenga bandari kavu, ikiwemo eneo la Kwala lililoko Ruvu mkoani Pwani na Katosho mkoani Kigoma.

Evariste Ndayishimiye, Rais wa Burundi

Akizungumzia suala hilo, Rais Ndayishimiye amesema, likikamilika litawapunguzia wananchi wa Burundi gharama ya usafirishaji mizigo na faini zinazotokana na biashara zao kukwama katika Bandari ya Dar es Salaam.

Rais Samia alitaja jambo la nne, ambalo ni ushirikiano katika sekta ya mawasiliano, ambapo Tanzania imetoa wito kwa Burundi kuutumia mkongo wake wa taifa wa mawasiliano ili kujitangaza kimataifa na kuvutia wawekezaji.

Jambo la tano ni ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, ambapo wamekubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara ikiwemo vilivyotokana na janga la Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), ili kupandisha thamani ya baishara ya nchi hizo mbili iliyofikia Sh. 200 bilioni mwaka 2019.

Rais Samia alitaja jambo la sita kuwa ni ombi la Tanzania kwa Serikali ya Burundi, kuanza kutumia mfumo wa malipo wa Afrika Mashariki, ambao magavana wa nchi hizo mbili wameagizwa kuzungumza ili kufanya utekelezaji wake.

Katika jambo la saba, Rais Samia amesema Serikali ya Burundi imekubali kuipatia msaada wa mbolea Serikali ya Tanzania, ili kuwasaidia wakulima hususan katika kipindi ambako kuna uhaba wa bidhaa hiyo duniani.

Rais Samia alitaja jambo la nane ambalo ni, ushirikiano wa mataifa hayo mawili kwenye sekta ya afya, ambapo Tanzania iliiomba Burundi kutumia huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo na kansa zinazotolewa nchini.

Jambo la tisa alilotaja Rais Samia, ni uimarishwaji ushirikiano baina ya vyama tawala vya nchi hizo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), cha nchini Tanzania na CNDD-FDD cha Burundi.

“Tumekubaliana kuweka mahusiano makubwa kwenye vyama vyetu vya siasa, vyama vinavyotawala nchi yetu, Chama Cha Mapinduzi na Chama cha National Council for the  Defence of Democrasy (CNDD-FDD),” amesema Rais Samia.

Jambo la 10 lilitajwa na Rais Ndayishimiye, aliyesema Burundi itajifunza utaalamu juu ya namna ya kuendesha sekta ya madini kutoka nchini Tanzania, ambapo mataifa hayo mawili yamesaini hati ya makubaliano ya ushrikiano katika sekta hiyo.

Pia, Rais Ndayishimiye amesema Burundi itanunua makaa ya mawe kutoka Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!