August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

TANTRADE yatakiwa kujiwekea malengo, kutoa elimu masoko

Spread the love

 

MAMLAKA ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imetakiwa kujiwekea malengo kwa kila maonyesho na baadae kufanya tathimini ya kufanikiwa au tutofanikiwa. Anaripoti Jonas Mushi Dar es Salaam … (endelea).

Maagizo hayo yametolewa leo Jumatano tarehe 13 Julai, 2022, na Mkamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akifunga maonesho ya 46 ya kimataifa ya biashara maarufu SabaSaba.

Dk. Mpango amesema bila uwepo wa malengo haiwezi kutathimini endapo imefanikiwa au la na pia kujilinganisha na maonesho emngine ya kimataifa.

Ameitaka pia kuweka malengo na mipango hiyo kwenye tovuti yao pamoja na taarifa ya tathimini ya kila maonesho.

“Mwaka jana niliwaomba TANTRADE muwe na utaratibu wa kujiwekea malengo ili muweze kujipima mmefanikiwa au mmeshindwa kiasi gani na muweze kujilinganisha na maonesho mengine ya kimataifa.

“Mmejaribu kidogo lakini naomba muyaweke kwenye tovuti yenu na mmejishtaki maana nimetembelea tovuti yenu kwenye maeneo ya mpango mkakati na malengo ya mwaka vipo tupu lakini pia katika machapisho sijaona kitabu kuhusu tathimini ya maonesho yaliyopita,” amesema Mpango na kuongeza;

“Natoa tena rai kwenu mlitafakari hili naamini ni jambo zuri la kulifanyia kazi.”

Pia ameitaka ikusanye maoni kwa washiriki wa maonesho na wadau mbalimbali ili iweze kuboresha zaidi maonesho yanayofuata.

Mbali na hayo amesema pamoja na jitihada za kuondoa ushuru wa forodha na kuweka vivutio mbalimbali ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za nafaka, nyama, samaki, matunda na mbogamboga, bado kiwango cha biashara kikanda ipo chini ya asilimia 20.

“Napenda kuwasihi tutumie fursa hizi katika kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa zetu pamoja na kuangalia kikamilifu kuuza katika eneo huru la biashara la Afrika ambalo lina takribani watu bilioni 1.3.”

Kutokana na changamoto hiyo Dk. Mpango amemwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE na wizara zote za bara na Zanzibar kutoa elimu zaidi kuhusu masoko hayo kwa wafanyabiashara ili waweze kuchangamkia fursa hizo.

Aidha ameiagiza Wizara ya Viwanda, biashara na Uwekezaji kubaini vikwazo vya biashara baina ya Tanzania na nchi zingine za bara la Afrika.

Pia ameagiza Wizara ishirikiane na wafanyabiashara pamoja na taasisi ya sekta binafsi kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Rais kwa taasisi zote za Serikali kuhusu kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchi.

“Fuatilieni kwa karibu kuona kama kweli urasimu upo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vibali vya biashara au uwekezaji nchini tuhakikishe urasimu unaondolea kama ilivyoanishwa kwenye mkakati wa kuboresha mazingira ya biashara,” amesema Dk. Mpango.

error: Content is protected !!