October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Takukuru yaokoa Bil 4

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jenerali John Mbungo

Spread the love

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), imeeleza kufanikiwa kuokoa zaidi ya Sh. 4 Bil baada ya kufanyia kazi ripoti ya ukaguzi wa vyama vya ushirika. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea). 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo tarehe 22 Januari 2020, Jenerali John Mbung’o, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo amesema, wameokoa pesa hizo kati ya bilioni 51 walizozichunguza ndani ya mwezi mmoja na nusu.

Na kwamba, ni tangu wapokee muhtasari wa uchambuzi wa ukaguzi kwa vyama vya ushirika kwa mwaka wa fedha 2018/19, kutoka kwa Japheth Hasunga, Waziri wa Kilimo tarehe 26 Novemba 2019, jijini Dodoma.

Amesema, ukaguzi huo ni awamu ya kwanza uliofanywa na Takukuru, ambapo mpaka sasa umefanikiwa kuchunguza kiasi cha Sh. 51, 794,222,683.09 na kwamba, uchunguzi wa Sh. 72, 259, 029,190.91 kwa awamu ya pili, unaendelea vizuri.

“Katika ufuatiliaji huo, Takukuru imefanikiwa kuokoa kiasi cha 4,066,162,092.38 ambazo baadhi zimerejeshwa kwa wakulima na vyama vya ushirika, ama kutunzwa katika akaunti maalumu zilizofunguliwa kwa ushauri wa warajisi wa vyama hivyo na wakuu wa mikoa,” amesema.

Amesema, kwa mujibu wa muhtasari wa taarifa iliyokabidhiwa Takukuru jumla ya fedha ambazo zilikuwa na viashiria vya ubadhirifu pamoja na rushwa ni zaidi ya bilioni 124 na kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2019 vyama vilivyodajiliwa vilikuwa 11,410, kati ya hivyo, vyama hai ni 6,463  na vyama sinzia ni 2,844 lakini pia vyama ambavyo havipatikani au havijulikani vilipo nu 2,103.

“Alipokabidhi taarifa hii, Waziri wa Kilimo alisema pamoja na kwamba kuna baadhi ya vyama vilipata hati safi, vilikuwepo vyama vilivyopata hati chafu ambazo zilihusishwa na hoja zenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha na mali pamoja na rushwa,” amesema.

Aidha, amesewataka wanaushirika wote nchini au mtu yoyote mwenye fedha za ushirika, wazirejeshe mara moja kwani katika awamu ya pili, kwenye ufuatiliaji wa fedha hizo, hawatakuwa na huruma na mtu yoyote aliye fisadi au aliyetumia rushwa kujipatia faida.

Na kwamba, hatua hiyo itafanyika kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashitaka, na akaunti zote zitasimamishwa ama kutaifishwa mali zao.

error: Content is protected !!