October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Chadema: Wimbo wa CCM watibua mahakama

Viongozi wa Chadema wakijadiliana na wakili wao mahakamani Kisutu katika muendelezo wa kesi yao

Spread the love

WIMBO unaotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye shughuli zake za kampeni, unashawishi wananchi kuwanyima kura wapinzani. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Bonifac Jacobo, Meya wa Ubungo, jijini Dar es Salaam tarehe 22 Januari 2020, wakati akitoa ushahidi wake kwenye kesi ya uchochezi namba 112/2018, inayowakabilia viongozi tisa wa Chadema.

“Huo wimbo umeimbwa na Marehemu Kapteni Komba, unaimbwa ‘Harambee mara tatu, kisha wanaimba ‘wapinzani tuwalete, tuwachanechane tuwatupe… CCM tuwalete tuwakumbatie tuwabusu.” Meya Jacob amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, wakati akitoa ushahidi wake.

Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo, alitoa maelezo hayo baada ya kuongozwa na wakili wa utetezi Peter Kibatala, aeleze maneno yaliyotumika kwenye uchaguzi kuhusu ‘kichonjio’ (kitambulisho cha kura).

Viongozi wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema  – Taifa; Salum Mwalim, Naibu Katibu Mkuu Chadema – Zanzibar; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini; Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Wengine ni John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema; Vicent Mashinji, aliyekuwa Katibu Mkuu na Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini.

Jacobo ambaye ni shahidi wa 10, akiongozwa na wakili Kibatala mbele ya Hakimu Thomas Simba, ameieleza mahakama kuwa yeye (Jacobo), ndiye aliyekuwa mshereheshaji kwenye kampeni za uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni, tarehe 16 Februri 2018.

Wakili Kibatala alimuuliza Jacob kuhusu ufahamu wake kwenye lugha ya kampeni za kisiasa, maana ya kuchinja na kichinjio amejibu.

Hata hivyo, alijibu “kuchinja ni kumnyima mtu kura na kichinjio ni kitambulisho cha kupiga kura.” Na kisha alimuuliza kuhusu ufahamu juu ya  wimbo huo ulioimbwa na Marehemu Kapteni Komba.

Wakati mahojiano yakiendelea, Faraja Nchimbi, wakili wa serikali mkuu alisimama na kumuomba Hakimu Simba amuongoze wakiki Kibatala, kutouliza maswali kuhusu wimbo huo, kwa kuwa hauhusiani na shauri hilo.

Wakili Nchimbi alipinga swali kuhusu wimbo huo kwa madai, hauna uhusiano na shauri hilo, lakini Hakimu Simba aliruhusu swali hilo kuendelea kuulizwa.

Hata hivyo, hoja ya wakili Nchimbi ilijibiwa na wakili Kibatala kwamba, anazo sababu za msingi kuanza kuhoji kuhusu wimbo huo, “huu wimbo umeimbwa na mtu mwengine, na nina hoja ya kisheria kwenye hili.”

Kutokana na mvutano uliokuwepo kuhusu wimbo huo, Hakimu Simba aliamua kuahirisha shauri hilo kwa muda, ili pande mbili zikajipange na kukubaliana na kisha shauri likaendelea.

Hakimu Simba alitoa takribani dakika 10, kuhakikisha kunakuwa na maelewamo kati ya pande mbili. Baada ya dakika takribani 10, Hakimu Simba alirejea kwenye chumba namba 2 chama hmahakama hiyo kuendelea kusikiliza shauri hilo. Hoja zikaendelea.

error: Content is protected !!