KUFUATIA ajali ya basi la shule ya msingi ya Ghati Memorial, iliyogharimu maisha ya wanafunzi nane, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeishauri Serikali itunge sheria na sera kali zitakazosaidia kutokomeza ajali hizo zinazosababishwa na uzembe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kama vile kupoteza maisha kwa ajali za kizembe na hata kubakwa na kulawitiwa, kwa kuwa hakuna sera na sheria zinazowabana wamiliki wa shule kuajiri watu wenye sifa sahihi za kuhudumia watoto.
“Sasa tumeona anachukuliwa dereva, mtumishi na mwalimu hana mafunzo yoyote ya mtoto, hana nidhamu ya kukaa na mtoto mwisho wa siku ndio haya yanayotokea madereva wanaua watoto, wanabaka watoto na matukio mengi yanakwenda kuwadhalilisha watoto tunapaswa kuwalinda watoto,” amesema Olengurumwa.
Olengurumwa amesema “sisi watetezi wa haki za binadamu tunaishauri Serikali ije na sheria na sera za kuwalinda watoto wanapokuwa katika mikono ya taasisi hizo, ili tuhakikishe tunaweka mazingira salama ya kukua na kupata maarifa kwa ajili ya taifa la kesho.”
Olengurumwa amesema sheria na sera zikitungwa zitaweka utaratibu juu ya namna ya kupata watumishi wa shule wanaofaa na wanaozingatia sheria, badala ya hali iliyopo sasa ambapo mmiliki anaajiri mtu yeyote hata kama hana mafunzo juu ya namna ya kulea na kuhudumia watoto.
“Tunapoangalia malezi ya watoto tuangalie zile taasisi zinazohusiana na malezi tumeweka kanuni na sheria zipi kuzisimamia? Kuanzia tunavyoweza kuwapata watumishi wake, walimu, madereva na wengine. Tuna utaratibu gani tunaotumia kuwapata? Je, tunawapa mafunzo gani kuhusiana na usimamizi na ulinzi wa mtoto? nasisitiza tuwe na utaratibu mzuri wa kuwapata watumishi,” amesema Olengurumwa.
Ajali hiyo iliyokea mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo chanzo kinadaiwa ni uzembe wa dereva aliyelazimisha kutaka kupita katika maji yanayokwenda kasi, kisha basi kutumbukizwa korongoni.
Leave a comment