October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Serikali imuenzi Mkapa kwa utawala bora’

Hayati Benjamin Mkapa

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa wito kwa serikali kumuenzi Hayati Benjamin Mkapa katika dhana yake ya utawala bora. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na wanahabari John Mrema, Mkuu wa Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, amesema katika mambo matatu wanayopaswa kumuenzi Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia leo tarehe 24 Julai 202, jambo la kwanza ni uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Rais Mkapa ameandika kitabu chake, na tungetaka watawala wazingatia mambo yafuatayo, ameandika kuna haja ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kama watawala wanataka kuenzi wosia wake wakatekeleze hilo kwamba nchi hii inataka Tume Huru na tunaingia kwenye uchaguzi,” amesema Mrema.

 Akitaja jambo la pili, Mrema amesema ni kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mahusiano ya kimataifa.

John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema

“Rais Mkapa aliasisi diplomasia ya uchumi, wote mnakumbuka nchi yetu imerudi nyuma kwenye upande wa diplomasia, kama wanataka kumuenzi kuna haja ya kuenzi diplomasia na mahusiano ya kimataifa. Viongozi watoke wazungumze wengine sisi sio kijiji,” amesema Mrema.

Na jambo la tatu amesema, ili serikali imuenzi Mzee Mkapa basi isimame kwenye utawala bora.

“Tungependa viongozi wetu wajifunze, alijutia mauaji yaliyofanyika Zanzibar mwaka 2001 kama akiwa rais, majuto haya yakawe funzo kwamba kuna maisha baada ya kukaa madarakani, mwaka jana kwenye kitabu chake alisema kitu kinachomuumiza katika utawala wake ni kuhusu mauaji ya Zanzibar,” amesema Mrema.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Humphrey Polepole, Katibu Mwenezi wake, kimesema kimepokea kwa mshtuko kifo cha mwenyekiti wake huyo mstaafu.

“CCM kimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Ndugu Rais Mkapa, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM awamu ya Tatu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya Tatu,” inaeleza taarifa ya CCM.

Chama Cha Wananchi (CUF), kilichokuwa chama kikuu cha upinzani enzi za uongozi wa Rais Mkapa, kimesema kitakumbuka ujasiri wa Rais Mkapa hususan kupitia hatua yake ya kukiri hadharani udhaifu uliojitokeza katika uongozi wake.

Taarifa hiyo ya CUF imetolewa leo na Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.

“Kupitia kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ kilichozinduliwa mwaka jana, marehemu Mkapa alidhihirisha kujutia makosa yake na kutumia kitabu hicho kuliweka hilo bayana,” inaeleza taarifa ya CUF.

Taarifa hiyo ya CUF inaeleza kuwa, Rais Mkapa  amekuwa mwalimu mzoefu wa kuwafundisha viongozi walioko madarakani kuchunga matumizi ya madaraka yao, ili kuepuka makosa yaliyotokea katika utawala wake, pamoja na kufundisha  umuhimu wa kukiri makosa na kujirekebisha.

 “CUF kinatoa wito kwa viongozi waliopo madarakani kwa ngazi zote, kujifunza kupitia maisha ya marehemu Rais  Mkapa, ili wayaendeleze mazuri yake,”inaeleza taarifa ya CUF.

Chama hicho kimesema kitaukumbuka mchango wa Rais Mkapa katika kufanya mapinduzi madogo ya kiuchumi na uwekezaji enzi za utawala wake, pamoja na kuunda sera zilizosaidia Tanzania kusamehewa madeni makubwa kutoka kwenye mataifa tajiri.

error: Content is protected !!