September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Selasini ajiuzulu bungeni

Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo

Spread the love

JOSEPH Roman Selasini, Mbunge wa Rombo (Chadema), amejiuzulu nafasi ya unadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Selasini amechukua hatua hiyo leo tarehe 13 Januari 2020, ambapo ameandikia barua kwenda kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Kwenye barua yake, Selasini amedai, ni kutokana na kutopewa barua rasmi ya kukaimu nafasi hiyo iliyoshikiliwa na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho kabla ya kupigwa risasi na kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya kutafakari kwa kipindi chote nilichoitumia nafasi hii, hadi sasa ninapoandika barua hii na kwa miaka yote miwili, hujawahi kunipa barua rasmi ya kukaimu nafasi hiyo na kuthibitisha katika utumishi huo.

“Vilevile hujawahi kunipa onyo lolote la mdomo au maandishi kuonyesha kuwa, huridhiki na utendaji wangu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza:

“Na kwakuwa ofisi ya Katibu wa Bunge haina uthibitisho wowote wa mdomo au maandishi wa mimi kukaimu nafasi hiyo, ninakutaarifu kwamba, nimejiuzulu nafasi hii kuanzia tarehe ya barua hii.”

Katika barua hiyo ambayo nakala imeelekezwa kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai na Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai, Selasini amedai kuwa, amejiuzulu ili ampe nafasi Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, kufanya uamuzi wa kumteua mbunge mwingine atakayewaongoza katika kipindi kilichobakia cha uhai wa Bunge hilo.

Aidha, amemshukuru kiongozi huyo wa upinzani kwa imani ya kumteua kukaimu nafasi ya Lissu na kuwa, licha ya kuwasimamia wabunge wenzake, uteuzi wa nafasi hiyo ulimpa fursa ya kuhudhuria na kumuwakilisha katika kamati mbili muhimu bungeni ambazo ni Kamati ya Uongozi na Kamati ya Kanuni.

error: Content is protected !!