April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ya Meya Dar yafutwa, yamwacha na gharama

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imefuta kwa gharama, kesi namba tatu ya mwaka 2020 ya Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).

Mwita alifungua kesi hiyo tarehe 6 Januari 2020 dhidi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya ombi lake la kuzuia kuondolewa kwenye nafasi ya umeya.

Ombi la kuondoa shauri hilo, limewasilishwa leo tarehe 13 Januari 2020, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega na wakili wake Hekima Mwasipu.

Wakili Mwasapu amedai, upande wa mwombaji (Mwita) umeona shauri hilo halina maana kwa sababu, muombaji hajapewa haki yake ya msingi ya kusikilizwa.

Amedai, waliiomba mahakama kutoa amri ya kuzuia mchakato wa kumuondoa Mwita kwenye nafasi yake kabla ya uamuzi, lakini halmashauri ya jiji imefikia azimio la kumwondoa muombaji.

Akijibu ombi hilo, wakili wa serikali Rashid Mohamed, amedai kuwa hakuna pingamizi juu ya ombi hilo, isipokua mahakama ifute shauri hilo kwa gharama, kwani zimetumika rasilimali, muda na uwepo wao umegharimu.

Wakili Mwasipu amepinga hoja hiyo kwa kudai, rasilimali pamoja na muda ni kodi za wananchi ziendazo serikalini, hivyo wanaomba shauri hilo lifutwe bila gharama.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mtega amesema kuwa, mahakama hiyo imekubali ombi la mwombaji, na hivyo shauri hilo limeondolewa kwa gharama.

error: Content is protected !!