December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Simulizi za vifo Singida – Abdul Nondo

Spread the love

ABDUL Nondo, Mwanaharakati wa Haki za Binadamu amefanya utafiti mfupi kuhusu huduma ya afya katika Kata ya Iyumbu, Wilaya ya Ikungi mkoani Singida. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Akizungumza na wanahabari tarehe 13 Januari 2020, jijini Dar es Salaam kuhusu utafiti huo, Nondo amesema, kuna hali isiyoridhisha katika utoaji wa huduma hiyo huku vifo vya kizembe vikisababishwa na zahanati bubu.

“Uwepo wa zahanati bubu kumesababisha na kunaendelea kusababisha madhara makubwa kwa wananchi wa eneo lile, kwani wanaotoa huduma hizo hawana ujuzi zaidi ya kuwa na cheti cha kuuzia dawa baridi/muhimu.

“Hao ndio wanaenda mbali hadi kuchoma sindano, kupima magonjwa mbalimbali, kuzalisha chini ya mkeka,” amesema Nondo.

Akizungumzia madhila hayo, Nondo amesema kina ama wajawazito hulazimika kujifungulia chini ya mkeka, wakati mwingine (mama na mtoto) hupoteza maisha kwa kukosa rufaa pamoja na matibabu husika.

“Tarehe 18/11/2019 kuna mototo anayeitwa Msele Emmanuel, aling’atwa na mbwa akapelekwa duka la dawa (analitaja) ambapo ni zahanati bubu, mtoto akachomwa sindano ya PPF, baadaye mtoto akaanza kubweka.

“Walipomrudisha alipochoea sindano, wakaambiwa wampeleke Kituo cha Mzalendo ili wapewe rufaa kwenda mjini, yule mtoto alifia njiani. Mtaalamu wa afya angetambua mapema kwamba mtoto huyo anapaswa kupewa ant-rebies, hivyo anapaswa kupewa rufaa haraka kwenda mjini na sio kuchomwa sindano ya PPF,” amesema Nondo na kuongeza;

Pia ameelezea kifo cha Chiku Kimbuyi kilichotokea tarehe 24 Desemba 2019, kwamba mama huyu alikuwa mjamzito wa mimba ya miezi tano.

Alipelekwa kwa duka lile lile la dawa ambalo ni zahanati bunu akalazwa katika mkeka. Akaambiwa uchungu bado na ndipo muuguzi akaenda kunywa pombe, yule mama alitokwa na damu hadi kufariki.

Akizungumzia kunusurika kifo cha mke wa Said Miyunge, mkazi wa eneo hilo amesema, mwanamke huyo ambaye ni kijana wa pale Iyumbi ,alipelekwa kwenye zahanati hiyo bubu kujifungua.

Baada ya kujifungua, mke wa Said Miyunge alipatwa na kifafa cha mimba, walimrudisha haraka kwa muuguzi huyo.

Muuguzi huyo akakimbia na kujificha, ilibidi wampeleke kituo cha mzalendo haraka, wakapewa barua ya rufaa wakaenda kutibiwa mjini kwa muda, mke wake Said Miyunge akapona,” amesema.

Nondo amesema, tarehe 11 Januari 2020, muuguzi wa zahanati hiyo bubu alimuacha mjamzito katika duka lake (zahanati bubu), akatoka bila kueleza anakwenda wapi.

“Alipoondoka tu, mama yule alipatwa na uchungu, akaomba msaada huku mtoto akizaliwa chini ya mkeka,” amesema na kuongeza “watumishi wa kituo binafsi cha mzalendo, waliitwa kwenda kutoa msaada.”

Kifo kingine kilitokea tarehe 04 Julai 2019. Kwenye zahanati moja bubu ambapo amesema, muuguzi wa zahanati hiyo alimzalisha mama mjamzito ambapo alitoa mtoto mmoja na kuacha mtoto mwingine tumboni.

Nondo ameshauri serikali ifanye uchunguzi wa kina dhidi ya watumishi wa serikali wa wilaya hata mkoa wa Singida, kwamba wanaoshirikiana kwa kuwalinda zahanati bubu.

error: Content is protected !!