RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kesho tarehe 10 Juni 2021, anatarajia kuzungumza na Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, katika Ikulu ya jijini Dar es Salaam. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 9 Juni 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, akizungumzia ziara ya kikazi ya siku mbili ya Rais Masisi, nchini, inayotarajiwa kuanza kesho.
Balozi Mulamula amesema, katika mazungumzo baina ya Rais Samia na Rais Masisi, masuala manne yatajadiliwa.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje Tanzania, amesema suala la kwanza ni uimarishaji mahusiano ya kibiashara na uchumi, baina ya mataifa hayo mawili, kupitia Tume ya Pamoja ya Tanzania na Botswana.
“Watazungumzia mahusiano yetu kibiashara na uchumi kati ya nchi hizi mbili, kupitia makubaliano tume ya pamoja. Zitaimarisha biashara na uwekezaji .
Tanzania itauza mazao ya chakula kama soya, mchele, mafuta ya alizeti na viungo vya chakula Botswana. Pia tutawauzia mazao ya bahari, kwani wao hawana bahari,” amesema Balozi Mulamula.
Suala la pili lililotajwa na Balozi Mulamula, ni umarishwaji wa mahusiano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hasa masuala ya ulinzi na usalama.
“Viongozi wetu watajadiliana namna ya kuongeza juhudi za SADC, katika kutafuta amani na usalama wa kudumu katika kanda yetu, itakumbuwa Botswana ni mwenyekiti wa kamati inayosimamia masuala ya siasa, ulinzi na usalama,” amesema Balozi Mulamula.

Suala la tatu lililotajwa na Balozi Mulamula ni, ukuzaji lugha ya Kiswahili nchini Botswana, kwa Tanzania kupeleka watalaamu, kwa ajili ya kufundisha katika vyuo vikuu na watalaamu wa mambo ya nje wa Taifa hilo.
“Viongozi wetu wataweza zungumzia masuala ya diplomasia na matumizi ya lugha ya Kiswahili Botswana. Mtakumbuka 2019 ilipofanyika kikao cha wakuu wa nchi za SADC, azimio kubwa lililotokana na kikao hicho ni kuendeleza lugha ya Kiswahili,” amesema Balozi Mulamula.
Mwanadiplomasia huyo ameongeza “Botswana walipokea hili azimio kuona jinsi gani wataanzisha mitaala ya Kiswahili vyuo vikuu, kuiendeleza katika mawasiliano ya wizara ya mambo ya nje, tuna amini nalo litajitokeza, kuona jinsi gani Botswana inakuza matumizi yake.”
Suala la mwisho na viongozi hao kujadiliana mikakati ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona (Covid-19).
Leave a comment