June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Samia aendelea kupanga safu ya uongozi CCM

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameendelea kupanga safu ya uongozi wa chama hicho, tangu alipokabidhiwa wadhifa huo, mwishoni mwa Aprili 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Samia alikabidhiwa wadhifa huo, akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam. Mwili wake ulizikwa Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi mwaka huu.

Jana tarehe 29 Julai 2021, kikao maalumu cha Kamati Kuu ya CCM, kilichoketi jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Samia, kiliteua makatibu wakuu wa jumuiya mbili za chama hicho.

Ambapo, Gilbert Kalima, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho na Dk. Philipe Nyimbi, akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT).

Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Taarifa ya teuzi hizo, ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Shaka Hamdu Shaka.

Kabla ya uteuzi huo, nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, ilikuwa inashikiliwa na Erasto Sima, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo 2018. Wakati nafasi ya Katibu Mkuu UWT, ilikuwa ikishikiliwa na Queen Mlozi.

Uteuzi wa makatibu wakuu hao, unakuja mwezi mmoja, baada ya tarehe 22 Julai 2021, Kamati Kuu ya CCM kumteua Kenan Kihongosi, kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).

Kihongosi aliteuliwa kuchukua nafasi hiyo, akimrithi Raymond Mangwala, aliyeteuliwa na Rais Samia, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro.

Hadi sasa safu ya uongozi wa UVCCM haijakamilika, baada ya nafasi ya uenyekiti wa umoja huo iliyokuwa inashikiliwa na Kherry James, kuwa wazi kufuatia hatua ya Rais Samia kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam.

Mara baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa CCM, tarehe 29 Aprili 2021, Samia ambaye ni Rais wa Awamu ya Sita wa Tanzania, alimteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Daniel Chongolo, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme, akimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara.

error: Content is protected !!