Thursday , 9 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Sakata la Escrow: Bil 26 zamuweka huru Sethi
Habari Mchanganyiko

Sakata la Escrow: Bil 26 zamuweka huru Sethi

Spread the love

 

MFANYABIASHARA Habinder Sethi, aliyesota rumande kwa miaka minne ( 2017 hadi 2021), ameachwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kwa sharti la kulipa Sh. 26.9 bilioni, ndani ya miezi 12. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Sethi ameachiwa huru leo Jumatano, tarehe 16 Juni 2021, baada ya kulipa Sh. 200 milioni, kati ya Sh. 26 bilioni, alizokubali kulipa kwenye mazungumzo ya makubaliano ya kisheria (Plea Bagain), aliyofanya na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu.

Mazungumzo hayo yalikuwa ya kumaliza kesi ya uhujumu uchumi, iliyokuwa inamkabili na wenzake wawili, Mfanyabiashara James Rugemalira na Wakili wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania limited (IPTL), Joseph Makandege.

Akizungumza baada ya mfanyabishara huyo kuachiwa huru, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amesema Sethi atakuwa chini ya uangalizi wa kipindi cha miezi 12 na kwamba kuanzia leo hatakiwi kutenda kosa lolote.

Mbali na Sethi kulipa fedha za awali Sh. 200 milioni, Wakili Wankyo amesema, mfanyabiashara huyo ameiweka bondi kampuni ya IPTL, yenye namba za usajili 45566 na kiwanja namba 292/D, kilichopo maeneo ya Kunduchi Salasala, mkoani Dar es Salaam.

Wakili huyo mwandamizi wa Serikali, amesema Sethi alikutwa na hatia katika shitaka la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kiasi cha Dola za Marekani 22 milioni na Sh. 309.46 bilioni.

Baada ya Sethi kujitoa kupitia njia ya Plea Bargain, Wakili Wankyo amesema, Rugemalira na Wakili Makandege, wanaendelea kushtakiwa katika kesi hiyo.

Kwa sasa, Rugemalira na Wakili Makandege wanaendelea kukabiliwa na mashtaka 12, ikiwemo utakatishaji fedha, kula njama na kujihusisha na mtandao wa uhalifu.

Mengine ni, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, pamoja na kusababisha hasara kwa Serikali, zaidi ya Dola za Marekani 22 milioni na Sh, 309.46 bilioni.

Washtakiwa hao wadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya tarehe 18 Oktoba 2011 na tarehe 19 Machi 2014, jijini Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Rugemalira na Wakili Makandege.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia fedha kinyume cha sheria, katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa ajili ya utekelezaji wa mkataba wa ununuzi wa umeme na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Sakatala la Tegeta Escrow, liliibuka 2014 baada ya mabilioni fedha katika akaunti hiyo kuchotwa. Hali iliyosababisha kufanyika uchunguzi maalumu wa tukio hilo.

Kufuatia tukio hilo, tarehe29 Novemba 2014, Bunge kupitia mkutano wake wa 16/17, lilitoa maazimio yaliyosababisha mawaziri kadhaa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, kujiudhuru nyadhifa zao.

Mawaziri waliong’oka kutokana na sakata hilo ni, Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini pamoja na AG Fredrick Werema.

Wabunge waliovuliwa nyadhifa zao ni; Andrew Chenge (Bajeti- Bariadi Magharibi), William Ngeleja (Katika, Sheria na Utawala-Sengerema), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini-Lupa).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoMichezo

Kengold wakabidhiwa kombe NBC Championship

Spread the loveMdhamini mkuu wa Ligi Daraja la Kwanza (NBC Championship) Benki...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia: Matumizi ya nishati safi sio anasa, ladha ipo

Spread the loveRAIS Samia Suluhu Hassan amesema matumizi ya nishati safi kwa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

error: Content is protected !!