December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sabaya, wenzake kurejea tena mahakama kesho

Spread the love

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania, Lengai Ole Sabaya ambaye amehukumiwa miaka 30 gerezani, kesho Jumatatu tarehe 18 Oktoba 2021, atarejea tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kusikiliza kesi nyingine inayomkabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Sabaya mwenye miaka 34 na wenzake sita, wanakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi katika Mahakama hiyo ambayo Ijumaa iliyopita ya tarehe 15 Oktoba 2021, ilimhukumu kifungo hicho jela yeye pamoja na wenzake watatu.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, baada ya kumkuta na hatia Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura kwenye kesi iliyokuwa ikiwakabili ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Sabaya na wenzake walikuwa wanatuhumiwa kuvamia na kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha wa zaidi ya Sh. 2.7 milioni, katika duka la Mohamed Saad, tarehe 9 Februari 2021.

Pia, Sabaya na wenzake walikuwa wakituhumiwa kuiba Sh.390,000 kutoka kwa Bakari Msangi, Diwani wa Sombetini katika mtaa wa Bondeni.
Kesi hiyo, ilisikilizwa mfululizo kuanzia tarehe 19 Julai hadi 24 Agosti 2021 baada ya Sabaya na wenzake, kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo mhakamani hapo, tarehe 16 Julai 2021.

Aidha, walikuwa wakituhumiwa kuiba Sh.35,000 na simu ya mkononi aina ya Tecno ya Ramadhan Rashid wakiwa katika mtaa huo wa Bondeni ambapo makossa yote matatu walihukumiwa miaka 30 kila moja kwa maana ya miaka 90 kwa makossa yote. Hata hivyo, Hakimu Odira Amworo alisema watatumika makossa yote kwa miaka 30.

Wakati akiendelea kutumikia adhabu hiyo, kesho Jumatatu, atarejea tena mahakama hapo kuanza kusikilizwa mfululizo kwa kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi inamashtaka mbalimbali ikiwemo kuongoza genge la uhalifu pamoja na utakatishaji fedha inayomkabili Sabaya na wenzake sita ambao ni, John Aweyo, Watson Mwahomange, Enock Mnkeni, Sylvester Nyegu, Nathan Msuya na Jackson Macha.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wote wanatuhumiwa kujipatia Sh.90 milioni kutoka kwa
mfanyabiashara Fransis Mrosso kinyume na sheria.

Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kumsimamisha kazi tarehe 13 Mei 2021 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zinamkabili.

Sabaya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, alianza safari ya kuwa mkuu wa wilaya ya Hai, tarehe 28 Julai 2018 baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli, kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.

Katika uongozi wake ndani ya wilaya ya Hai, alikuwa akiendesha operesheni mbalimbali ambazo mara kadhaa zilikuwa zikilalamikiwa na wananchi pamoja na vyama vya siasa hususan Chadema kwamba zinakiuka misingi ya utawala bora.

error: Content is protected !!