Friday , 26 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sabaya ni funzo, azua mjadala
Habari za SiasaTangulizi

Sabaya ni funzo, azua mjadala

Lengai ole Sabaya
Spread the love

 

HATUA ya Serikali ya Tanzania, kumfikisha mahakamani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, imeibua mjadala mwingine wa kutaka kuwapo kwa uchunguzi mahususi juu ya minendo ya utumishi wa viongozi wa umma. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Sabaya na wenzake watano, walipandishwa mahakamani jana Ijumaa, tarehe 4 Juni 2021, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha na kusomewa mashtaka matano, likiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha.

Mashitaka mengine, ni uhujumu uchumi, utakatisha fedha, kushiriki vitendo vya rushwa na kuongoza magenge ya uhalifu.

Sabaya na wenzake, wamepelekwa kuhifadhiwa katika gereza kuu la Kisongo, mkoani Arusha, ambako watarejeshwa tena mahamani, tarehe 18 Juni, wakati kesi yao itakapotajwa tena.

Mashitaka yanayomkabili Sabaya, likiwamo la unyang’anyi wa kutumia silaha na utakatishaji fedha, hayana dhamana, huku mashitaka ya uhujumu uchumi, dhamana yake, inaamriwa kwa maombi anayopaswa kuyawasilisha Mahakama Kuu.

Mara baada ya Sabaya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili, baadhi ya wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida, walitoa maoni yao tofauti juu ya hatua hiyo.

Aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, kupitia ukurasa wake wa twitter, alimshauri Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan, aweke utaratibu mzuri wa watu kuripoti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, waliofanyiwa na baadhi ya wateule wa rais.

“Rais Samia nashauri uwekwe utaratibu maalumu, kwa watu waliofanyiwa vitendo vya ukiukaji wa haki zao, kupigwa, kuteswa kutishwa na wengine kunyang’anywa mali zao, ili waweze kutoa malalamiko yao,” ameeleza Msigwa.

Amesema, “hii itasaidia sana kuliponya taifa na kukomesha hi impunity (kutokujali), katika awamu ya tano.”

Naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, ameshauri kuundwa kwa Tume maalum ya Majaji, ambayo itapokea na kuchunguza malalamiko ya wananchi walioathirika na matendo ya wakuu wa wilaya, mikoa na watendaji wengine serikalini na katika vyombo vya usalama.

Zitto amependekeza kwa Rais, kwamba Tume atakayoiunda, iongozwe na mmoja wa majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufaa.

https://twitter.com/zittokabwe/status/1401033559645863937?s=19

Akiandika kutipitia ukurasa wake wa twitter, Zitto anasema, “tunataka iundwe Tume Maalum ya Majaji, itakayoongozwa na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, ili kupokea malalamiko ya watu wote walioumizwa,” amesisitiza mwanasiasa huyo.

Ameongeza, “Tume Maalum ya Majaji, itasikiliza na kuchunguza, malalamiko yote ya watu kuteswa, kubambikiwa kesi, kuporwa mali zao, kuuwawa, kutekwa na kupotezwa, ili haki iweze kutendeka.”

Kwa upande wake, mwanasheria na aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, amewashauri wateule wa rais na viongozi wa umma, kufuata sheria wawapo madarakani, ili kujiepusha na hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya Sabaya.

Amesema, “ushauri wangu kwa kila mtu aliyekabidhiwa madaraka, tukisema fuateni sheria na utaratibu na heshimu wananchi, mnatuona wapumbavu na mnatuita wasaliti.

Fatma ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume amesema kupitia ukurasa wake wa twitter, “kama bado hamuelewi awamu ni zama tu na kila zama ina mwanzo na mwisho wake, basi hamtojifunza milele. Haya sasa angalieni.”

Sabaya na wenzake wamefikishwa mahakamani, siku kadhaa baada ya kukamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), pamoja na vyombo vingine vya usalama.

Kukamatwa kwa Sabaya na kuhojiwa, kunafuatia maagizo ya Rais Samia aliyotoa tarehe 13 Mei mwaka huu.

Katika taarifa yake, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa, Rais Samia alisema, ameagiza Sabaya kusimishwa kazi, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Sabaya aliyeteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Hai, Julai mwaka 2018 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Pombe Magufuli.

Tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo, kumekuwapo na malalamiko lukuki kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara na wananchi wengine wa kawaida, kuhusiana na madai ya kuwapo “matendo ya kihalifu” ya kiongozi huyo.

Sabaya alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuendesha genge la ujambazi wa kutumia silaha, uporaji, utesaji na unyang’anyi, anaodaiwa kuutenda kwa nyakati tofauti.

Aidha, anadaiwa kuwaandika barua wafanyabiashara kadhaa na kuwalazimisha kumpatia mamilioni ya shilingi, kinyume na sheria.

Sabaya alikamatwa na kikosi kazi (Task Force), kinachohusisha taasisi mbalimbali za ulinzi na usalama.

Tayari kikosi kazi hicho, kimefanya mahojiano na watu kadhaa, katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, wakiwamo wahanga wa vitendo vyake.

Kabla ya kwenda Kilimanjaro, kikosi kazi hicho, kilikuwa mkoani Arusha, ambako kilikusanya ushahidi dhidi ya Sabaya.

Taarifa zinasema, wakati Sabaya anakamatwa alikuwa ameongozana na baadhi ya mabaunsa wake, wakiwamo wale waliohusika na uhalifu katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati Sabaya anakamatwa, alikuwa na magari matatu – moja likiwa linatumiwa na yeye mwenyewe na mawili yalikuwa yakitumiwa na wapambe wake.

Magari hayo yametambulika kuwa ni aina ya Toyota Harrier, Toyota Land Cruiser V8 zote nyeusi na Toyota Crown, yenye rangi nyeupe.

Mbali na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, Sabaya anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, ikiwamo kukusanya mamilioni ya shilingi kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara kwa matumizi yake binafsi.

Katika kutekeleza mradi huo, Sabaya amekitumia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kukusanya fedha akieleza kuwa baadhi ya fedha hizo, zinakwenda kufanyia shughuli za chama hicho tawala.

Mamilioni mengine ya shilingi yaliyokusanywa na Sabaya, yalielezwa kuwa yalikuwa yanatumika kwa shughuli za maendeleo wilayani Hai.

Hata hivyo, taarifa ndani zinasema, hakuna hata shilingi iliyokusanywa ilitumika kwa maendeleo ya Hai wala CCM.

Fedha zote zilizokusanywa ziliishia kwenye matanuzi yake.

Katika kipindi cha takribani miaka mitatu ya uongozi wake, maisha ya Sabaya yalikuwa yakitawaliwa na anasa na ubabe.

Baadhi ya watu waliokuwa wanamfahamu wanasema, alikuwa akiishi maisha ya anasa kuliko baadhi ya matajiri wakubwa nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

error: Content is protected !!