December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mambo matano yatikisa bajeti maliasili na utalii

Watalii wakiwa moja ya mbuga nchini Tanzania

Spread the love

 

MAMBO matano yameteka mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, uliotokea Ijumaa, tarehe 4 Juni 2021, bungeni jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mambo hayo ni pamoja na, kushuka kwa mapato ya sekta ya utalii, sheria ya kifuta machozi wananchi wanaoharibiwa mali zao na wanyamapori na ukata wa fedha za kutangaza vivuti vya utalii.

Mengine ni, migogoro ya mipaka ya makazi ya wananchi na hifadhi za wanyama pori na kudorora kwa vitalu vya uwindaji wanyamapori.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Mtama mkoani Lindi (CCM), Nape Nnauye, aliishauri Serikali itatue changamoto zinazokabili sekta ya utalii nchini, ili kupandisha mapato yatokanayo na sekta hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro

Nape alisema, mapato ya Serikali yatokanayo na uwindaji wa kitalii, yameshuka kutoka Dola za Marekani 27 milioni (2013), hadi 8 milioni (2019), pamoja na kampuni za utalii huo kupungua kutoka 60 hadi 40, katika kipindi hicho.

“Kuna maamuzi Serikali tulifanya, kubadilisha mfumo wa ugawaji vitalu, nia ni njema. Lengo ilikuwa kuondoa rushwa lakini mfumo iliyowekwa ina mapungufu, ndiyo maama vitalu mnapeleka mnadani vinakosa wateja,” amesema Nape na kuongeza:

“Kapitieni upya mfumo ulioanzishwa, mpunguze matatizo yaliyomo ikiwemo kuongeza uwazi. Hivyo mlivyoweka haitoshi, bado una mapungufu mengi ndiyo maana minada inakwama, minada inafanyika mnapeleka vitalu vingi mnauza vichache.”

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

Hoja ya ukata wa fedha za utangazaji vivutio vya utalii, iliibuliwa kwenye mjadala huo na Mbunge Viti Maalum (CCM), Riziki Rulida, aliyeiomba Serikali ielekeze nguvu zake kwenye kutangaza vivutio vya utalii vya nchi, kama zinavyofanya nchi nyingine barani Afrika.

“Kuhakikisha tunakuwa na Tanzania yenye mapato kupitia hifadhi na maliasili inawezekana, kwa kupitia mikutano ya kimataifa. Kule ndiko watu wanakwenda, niulize Tanapa waliwahi kwenda katika mikutano hiyo? Jibu hawana fedha. Lazima turudi nyuma, wenzetu wanatupita kwa kutangaza,” amesema Rulida.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa (Chadema), Aida Khenani, alisema wananchi wa jimbo lake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya migogoro ya mipaka ya hifadhi ya mapori tengefu.

Khenani amesema, migogoro hiyo inaibuka mara kwa mara, kufuatia ongezeko la idadi ya watu, na kuishauri Serikali ipitie upya mipaka hiyo.

“Kwa sababu idadi ya watu inaongezeka, kuna haja kubwa kwa wizara kwenda kupitia mipaka hii upya, ukitazama maumivu ya wananchi wetu, wanaiono Serikali inaheshimu i wanyama kuliko binadamu. Lazima tundoe hiyo dhana.”

Ester Bulaya

Mbunge wa Liwale (CCM), Zubeir Kuchauka, ameshauri Serikali ifanyie marekebisho sheria inayoelekeza malipo ya kifuta machozi, kwa wananchi wanaoharibiwa mali zao na wanyama pori, ili iendane na wakati.

“Kuhusu suala la kifuta machozi, sheria yake ni ya muda mrefu sana. Tangu 1974 mtu alikuwa anapewa Sh. 500 au 1000, kiwango kile bado kipo hadi leo, sheria hii haiendani na wakati wa sasa,” amesema Kuchauka.

Akikazia hoja hiyo, Mbunge Viti Maalum asiye na chama bungeni, Ester Bulaya alisema tatizo la fidia kwa wananchi wanaoharibiwa mali zao na wanyamapori lipo nchi nzima, huku akilalamika kwamba, wanaoathirika hupewa fidia ndogo tena kwa kuchelewa.

“Hili tatizo la fidia imekuwa kero katika maeneo mengi na sio kidogo na fedha haitoki kwa wakati, mfano Bunda Mjini, Tembo wanaharibu mazao yao na wanaomba fidia lakini fidia yao hawaipati,” amesema Bulaya.

error: Content is protected !!