SERIKALI ya Tanzania, imetoa wito kwa wasomi, watafiti pamoja na wafanyabiashara wa nishati mbadala, kutafuta njia zitakazowawezesha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, ili kutokomeza tatizo la ukataji holela miti katika misitu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, tarehe 5 Juni 2021 na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, katika sherehe za maadhimisho ya siku ya mazingira duniani, zilizofanyika jijini Dodoma.
“Napenda kutoka wito kwa wafanyabiashara hasa wa gesi ya kupikia nyumbani na wadau wengine, waweze kubuni mbinu za kusaidia wananchi wa kipato cha chini, waweze kumudu gharama za nishati mbadala,” amesema Dk. Mpango.
Wakati huo huo, Dk. Mpango amewataka wadau wa nishati mbadala, kubuni miradi itakayoongeza matumizi ya nishati mbadala nchini, ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, yanayosababisha misitu kupotea kutokana na miti kukatwa.
“Wadau hatuna budi kuongeza nguvu kutekeleza miradi inayolenga kuongeza matumizi ya nishati mbadala, ikiwemo gesi asilia na vifaa vinavyotumia nishati kidogo katika kupika,” amesema Dk. Mpango.
Aidha, Dk. Mpango amesema Serikali itapitia upya viwango vya kodi kwa wafanyabaishara na wazalishaji wa nishati mbadala ikiwemo, gesi asilia, ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa ajili ya kuondolea mwananchi mzigo wa gharama za kupata nishati hizo.
“Tatizo kubwa kwetu ni namna gani tunapunguza bei ya nishati mbadala na bei ya jiko, niwasihi vyuo vyetu na watafiti wengine wafanye kazi kutafiti, kwa nini bei ya nishati mbadala inakuwa kubwa,”
“ Na nini kifanyike, kama kuangalia mfumo wa kodi tuutazame, lakini kama gharama ya kuzalisha nishati mbadala nazo ziweze kutazamwa,” amesema Dk. Mpango.
Makamu huyo wa Rais wa Tanzania, amesema matumizi ya kuni na mkaa katika shughuli za nyumbani na kwenye biashara, yanaendelea kuongezeka siku hadi siku, kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
Na kwamba, tafiti za mapato na matumizi ya kaya binafsi zilizofanywa kuanzia mwaka 2007 hadi 2018, zinaonesha katika kila kaya 100, 90 zinatumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia.
Amesema ongezeko la matumizi hayo, limesababisha vitendo vya ukataji miti kuongezeka, ambapo mkoa wa Dar es Salaam peke yake, unatumia heka 188 za misitu kila mwaka, kwa ajili ya kupata kuni na mkaa.
“Mfano Dar es Salaam wanatumia zaidi ya magunia 500,000 ya mkaa, kwa mwaka mmoja, sawa na tani 45,000, mita za ujazo wa miti 75,000. Kwa lugha nyepesi sawa na kukata heka 188 kila mwaka,” amesema Dk. Mpango na kuongeza:
“Hali hii kwa kweli inatia wasiwasi, maana imeanza kusababisha kupotea misitu yetu kwa haraka na kuvurugika mifumo ya ikolojia na hivyo kuongeza kasi ya kuenea hali ya jangwa na ukame katika nchi yetu.”
Leave a comment