May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ripoti ya CAG yamkaanga Dk. Kigwangalla

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangalla akikabidhi tuzo katika Tamasha la Urithi

Spread the love

 

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, imemuweka matatani aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akitoa muhtasari wa ripoti hiyo jijini Dodoma, leo Alhamisi tarehe 8 Aprili 2021, CAG Charles Kichere amesema, katika tamasha la Urithi Festival lililofanyika mwaka 2019, kulikuwa na viashiria vya ubadhirifu wa fedha kutokana na kanuni mbalimbali kukiukwa.

Tamasha hilo lilifanyika chini ya uongozi wa Dk. Kigwangalla wakati akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
CAG Kichere amesema, fedha zilizotumika kufanikisha tamasha hilo, hazikuwa katika bajeti ya wizara hiyo, wala hakukuwa na mpango ulioidhinishwa wa utekelezaji wake.

Amesema, kutokana na fedha hizo kuwa nje ya bajeti, wizara hiyo ilichangisha kiasi cha Sh. 1 Bil kutoka katika wakala zake nne ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wanyapori Tanzania (TAWA).

Charles Kichere, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)

“Kulikuwa hakuna mpango wa utekelezaji wa tamasha la utalii. Kutokana na kukosekana kwa mpango wa utekelezaji uliodhinishwa, nilibaini kuwa wizara ya malialsili na utalii iliomba wakala zake nne kuchangia.”

“Kila moja ilitakiwa kuchangia Sh. 250 Mil ambazo hazikuwa kwenye bajeti zao, ili kuwezesha kufanyika kwa tamasha hilo,” amesema CAG Kichere.

CAG Kichere amesema, ili kuongeza bajeti hiyo, wizara ilichangia Sh. 299 Mil na Mfuko wa Fedha za Maendeleo ya Utalii Sh. 270 Mil. Jumla Sh. 1.57 Bil zilipatikana ili kufanikisha utekelezaji wa tamasha hilo, ambao fedha hizo zilikuwa hazikuwa katika bajeti za wizara wala taasisi husika.

Licha ya hayo, CAG Kichere amesema, alibaini hakukuwa na stakabadhi zinazothibitisha malipo ya Sh. 831.1 Mil kutoka kwa wizara hiyo kwenda kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Wakati wa utekezaji nilibaini kuwa, kituo cha TV cha Clouds na TBC walichukua jumla Sh. 629.7 Mil na Sh. 201.4 Mil mtawalia. Kwa maana Clouds walilipwa Sh. 629.7 Mil na TBC Sh. 201.4 Mil kwa ajili ya kuonesha matangazo ya tamasha.”

“Hata hivyo, hakukuwa na risiti (stakabadhi) za kielekroniki kuthibitisha kupokelewa kwa malipo hayo na hao waliolipwa,” amesema CAG Kichere.

Pia amesema, katika sakata hilo, kodi ya zuio kiasi cha Sh. 41 Mil hazikukatwa katika malipo yaliyofanyika.

“Aidha, kodi ya zuio ya Sh. 31 Mil. na 10 Mil. kutoka Clouds TV na TBC mtawalia haikukatwa katika malipo yaliyofanywa.”

“Wizara haikupata hizo kodi ya zuio. Ushaidi unaonesha kuwa, manunuzi ya huduma za matangazo kwa TBC na Clouds, zilipatikana kwa njia ya ushindani usiosawa,” amesema CAG Kichere.

Pia, CAG Kichere amesema katika ukaguzi wake, alibaini kwamba matumizi ya Sh. 478.26 katika taasisi saba, hayakuwa na nyaraka.

“Nilibaini jumla Sh. 487.26 zilipelekwa kwenye taaissi saba kwa ajili ya utekelezaji wa tamasha hilo. Hata hivyo hakukuwa na nyaraka kwa ajili ya ukaguzi, kuthibitisha matumizi hayo,” amesema CAG Kichere.

Mkaguzi huyo wa hesabu za Serikali amesema “Hali kadhalika nilibaini matumizi ya Sh. 585.52 Mil. yaliyolipwa na mhasibu wa Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii bila kuwa na nyaraka toshelezi, hivyo nilishindwa kuthibitisha uhalali wa matumizi hayo.”

Katika hatua nyingine, CAG Kichere amesema katika ukaguzi wake alibaini kiasi cha Sh. 140 kilitolewa na wizara hiyo kwa maelekezo ya Dk. Kigwangalla kwenda Kampuni ya Wasafi, kinyume na Sheria ya Matumizi ya Umma.

Amesema, fedha hizo zililipwa kwa ajili ya wasanii wa kampuni hiyo kutangaza utalii wa ndani katika mikoa sita (Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Moshi-Kilimanjaro na Iringa).

“Nilibaini wizara ililipa Sh. 140 Mil Kampuni ya Wasafi kwa ajili ya wasanii ambao wangetangaza utalii wa ndani, hakukuwa na mkataba wowote uliosainiwa kati ya kampuni hiyo na wizara. Hivyo, sikuweza kuhakiki wigo wa kazi pamoja na huduma zilizotolewa na Kampuni ya Wasafi.

“Kulikuwa na maagizo ya waziri yakielekeza malipo kwa Kampuni ya Wasafi, katika mahojiano waziri alikiri kuwa, kampuni hiyo iliomba zabuni ya kutangaza tamasha hilo katika mikoa iliyotajwa, na kutoa maagizo ya kutolewa malipo hayo,” ameeleza.

Amesema, kwa maoni yake kiasi cha Sh. 140 Mil walicholipwa Wasafi kufuatia malekezo hayo, hakiendani na sheria ya matumizi ya umma.

error: Content is protected !!