SERIKALI ya Tanzania, imeeleza, katika kipindi cha miaka mitano (2019-2020), jumla ya viwanda vipya 8,477 vimejengwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kati ya hivyo, vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo zaidi 4,410, na kwamba ujenzi wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi viwanda 61,110.
Ni kauli ya Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango aliyoitoa leo Alhamisi tarehe 7 Aprili 2021, bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).

“Viwanda hivyo vimechangia ongezeko la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali katika soko la ndani na la nje ikijumuisha bidhaa za ngozi, nguo, ujenzi (nondo, mabati, saruji, misumari, marumaru na rangi), plastiki, zana za kilimo na vinywaji.”
“Uwekezaji huo umeleta mafanikio yafuatayo: Kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 7.9 mwaka 2015 hadi asilimia 8.5 mwaka 2019; kukua kwa sekta ya uzalishaji viwandani kwa wastani wa asilimia 8.3.
Akitaja mafanikio mengine amesema, viwanda hivyo vimesaidia kuzalishwa fursa za ajira kutoka ajira 254,786 mwaka 2015 hadi ajira 482,601 mwaka 2019 na kuchangia katika mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi kutoka asilimia 13.8 mwaka 2016/17 hadi asilimia 14.2 mwaka 2019/20.
Amesema, katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, Sh. 45.3 bilioni kimetumika kuchochea miradi ya uzalishaji viwandani.
Leave a comment