December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia azungumzia anguko la upinzani Uchaguzi 2020 Kilimanjaro

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewashukuru wananchi wa Kilimanjaro kwa kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, kwenye nafasi za urais, ubunge na udiwani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametoa pongezi hizo leo tarehe 15 Oktoba 2021, akizungumza na wananchi wa Kilimanjaro, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Rais Samia amesema wananchi wa Kilimanjaro walifanya kazi nzuri katika Uchaguzi Mkuu huo uliofanyika Oktoba 2020, kwa kuichagua CCM.

“Napenda kuwashukuru kwa kazi nzuri mliyoifanya mwezi wa 10 mwaka jana, wananchi wa Kilimanjaro mlituthibitishia mwaka jana kwamba ile likizo mliyoitoa kwa CCM iliisha, ile likizo ya kukaa bila maendeleo imeisha,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Na mkasema sasa tunataka maendeleo, kwa maana hiyo mkairudisha CCM madarakani, nawashukuru sana ile ili kuwa kazi nzuri sana.”

Kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo, majimbo mengi ya mkoa huo yalikuwa yanashikiliwa na vyama vya siasa vya upinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), pamoja na NCCR-Mageuzi.

Hata hivyo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, CCM kilifanikiwa kuzoa majimbo yote mkoani Kilimanjaro.

Si Kilimanjaro peke yake, CCM ilipata ushindi wa zaidi ya asilimia 90 kwenye uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani, ambapo vyama vya upinzani viliambulia majimbo manne kati ya majimbo zaidi ya 300.

error: Content is protected !!