December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aacha fumbo Moshi kuwa jiji

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaachia fumbo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwamba wachague moja kati ya Vunjo kupewa hadhi ya Halmashauri Mpya au Manispaa ya Moshi kuwa jiji. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 15 Oktoba, 2021 wakati akijibu ombi la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo ambaye amemuomba aipandishe hadhi Manispaa ya Moshi kuwa jiji.

Akizungumza katika ziara ya kikazi ya Rais Samia mkoani Kilimanjaro, Tarimo amesema licha ya kuwa Moshi ina eneo dogo, halmashauri hiyo inakusanya mapato mengi, hivyo ikipandishiwa hadhi kuwa jiji, itakusanya mapato mengi.

“Sisi tuko kwenye yale maeneo ambayo yanaomba kuongezewa hadhi, jimbo letu ndio jimbo dogo zaidi. Halmashauri yetu ina kilomita za mraba 58 tu, lakini katika hizo kilomita tuna makusanyo ya ndani Sh. bilioni tano mpaka bilioni 6,” amesema Tarimo na kuongeza:

“Lile tangazo la Serikali namba 219/2016 ambalo lilisainiwa tarehe 26 Juni 2016 na Waziri wa Ardhi, William Lukuvi kwamba Halmashauri inatarajiwa kupanuka kwa kuongezewa eneo la ardhi hadi kufikia kilomita za mraba 142 ili kuweza kuwa jiji, sasa tunaomba likamilike tuweze kuwa jiji tupate makusanyo zaidi na tuendelee kuijenga nchi yetu.”

Akijibu ombi hilo, Rais Samia amesema Serikali italifanyia kazi licha ya halmashauri hiyo kutokidhi vigezo vya kuwa jiji.

“Ndugu zangu hapa inabidi tuangalie vizuri, Mji wa Moshi unatakiwa kuwa jiji, lakini vilevile Vunjo wanataka kuwa halmashauri, ila ukitoka Moshi kwenda Vunjo si zaidi ya km 20 au 25. Sasa hapa aidha, Vunjo ivunjwe tufanye jiji au mseme tufanyeje,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Lakini pia kuna suala la vigezo ambalo tukiangalia bado Mji wa Moshi haijafikia, lakini niwaambie Serikali italifanyia kazi kuangalia yote, tuvunje Vunjo iingie jijini au jinsi tutakavyoona inafaa kulingana na vigezo vilivyopo.”

error: Content is protected !!