RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali leo Jumanne, tarehe 17 Agosti 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Taarifa iliyotolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imewataja walioteuliwa kuwa; ni Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).
Rais Samia, amefanya uteuzi huo akiwa nchini Malawi anakoendelea kushiriki mkutano wa 41 wa Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mkutano huo, umeanza leo Jumanne na utamazilika kesho Jumatano.
Pia, amemteua Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Kabla ya uteuzi huo, Prof. Ole Gabriel alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (upande wa Mifugo) ambaye anachukua nafasi ya Mathias Kabunduguru ambaye amestaafu.
Haniu amesema, Prof. Ole Gabriel ataapishwa tarehe 21 Agosti, 2021, saa 03:00 asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam pamoja na Mabalozi Wateule watatu.
Mabalozi hao; ni Lt. Jen. Yakub Hassan Mohamed kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Balozi mteule Mahmoud Thabit Kombo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na Balozi Mteule Elsie Sia Kanza kuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Leave a comment