May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ajitambulisha SADC, awapa ujumbe marais

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa SADC

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amehutubia mkutano wa 41 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kujitambulisha rasmi kwa Wakuu wa nchi na Serikali wa jumuiya hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Malawi … (endelea).

Amejitambulisha leo Jumanne, tarehe 17 Agosti 2021, katika mkutano wa SADC uliofanyika Lilongwe nchini Malawi. Mkutano huo unamalizika kesho Jumatano.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema Malawi ni Taifa la kwanza katika nchi za SADC kuongozwa na Rais mwanamke, hivyo kujitambulisha kwake katika mkutano huo kutaongeza msukumo kwa wanawake wengi zaidi kujiamini na kuhamasika kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.

Rais Samia amewasihi viongozi wa SADC kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kuwainua na kuwawezesha wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika nchi zao.

Aidha, Rais amewafahamisha viongozi wa SADC kuwa katika mkutano wa Generation equality uliofanyika hivi karibuni nchini Ufaransa ulimchagua kuwa kinara (champion) wa masuala ya haki za kiuchumi za wanawake (Women Economic Rights and Justice), hivyo kuomba ushirikiano kutoka kwao ili yeye na timu yake iweze kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.

Amesema katika kipindi cha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa SADC kumekuwa na mafanikio na changamoto mbalimbali, hivyo akiwa ni kiongozi mpya katika Jumuiya hiyo ameahidi kutoa ushirikiano ili kusukuma ajenda za utengamano, kushughulikia changamoto na kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumzia kuhusu kukabiliana na janga la UVIKO – 19, Rais Samia amesema lengo la Serikali yake ni kuhakikisha wananchi wote wanachanjwa ili kupata kinga ya ugonjwa huo.

Ameziomba nchi za SADC kushawishi kampuni zinazozalisha chanjo kuridhia vibali na teknolojia zao zitumike ili kuruhusu chanjo kuzalishwa katika nchi mbalimbali ili kukidhi mahitaji yaliyopo.

Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia amesema ni lazima kushirikiana katika kubadilishana mbinu na uzoefu na kuwaelimisha wananchi kuhusu dhana potofu dhidi ya chanjo hizo pamoja na kuwahimiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na janga hilo.

Pia ameziomba Nchi zilizoendelea na Taasisi za Kifedha za Kimataifa kuendelea kutoa misamaha au kurefusha muda wa ulipaji wa madeni kwa Nchi zinazoendelea mpaka pale janga hilo litakapokwisha.

Rais Samia amempongeza Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa SADC na pia amempongeza Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi kwa kazi kubwa na nzuri ya kuingoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Vilevile, Rais Samia amempongeza Katibu Mtendaji wa SADC, anayemaliza muda wake Dk. Stagomena Tax kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye Jumuiya hiyo kwa kipindi cha uongozi wake ambapo ameiwakilisha vyema Tanzania katika Jumuiya hiyo.

error: Content is protected !!