October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aonya migogoro Kanisa Anglikana

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi wa dini wa Kanisa la Anglikana Tanzania kurudi kwenye misingi ya kimaadili ya kanisa na kumaliza mizozo inayoibuka kila mara ndani ya kanisa hilo. Anaripoti Glory Massamu – TUDARCo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 28 Septemba jijini Dodoma wakati akihutubia kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Anglikana tangu lipate usajili wa kudumu hapa nchini.

Akinukuu ubeti wa pili na wa tatu uliopo katika moja ya nyimbo za kanisa hilo, Rais Samia amesema licha ya kwamba wimbo huo unasisitiza umoja na mshikamano anashangaa kuona kila mara anasikia migogoro ndani ya kanisa hilo.

“Nimevutiwa na ule wimbo tulioanza nao, ni mzuri sana, nimevutiwa na ubeti wa pili na wa tatu. Lakini najiuliza kila mtu anauimba kutoka moyoni, anaamini anachokiimba, kama ni hivyo mbona tunasikia papapa! za hapa na pale ndani ya kanisa la Anglikana!

“Wenyewe mnasema majaribu yapo mengi na adui ni nje na ndani, mbona hamponyani? mbona tunasikia mizozo? ile kazi yetu kama viongozi wa dini kujenga umoja, mshikamano na upendo, itafanyika kwenye mizozo hii? naomba turudi kwenye ule wimbo tuuimbe kwa dhati na tuuamini,” amesema Rais Samia.

Aidha, Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa amesema kanisa hilo limeendelea kukua kwani tangu lilipopata usajili hapa nchini lilikuwa na dayosisi nane lakini sasa lina dayosisi 28.

Amesema licha ya kwamba kanisa hilo lenye miaka 176 tangu lilipoingia nchini limechangia kuboresha huduma za afya kwa kuwa na vituo vya afya 40 na vyuo vya afya saba bado kuna changamoto ya kodi ya serikali katika utoaji wa huduma hizo za afya.

Amesema kwa upande wa elimu kuna taasisi za elimu 63 ikiwamo Chuo kikuu cha St. John Dodoma.

Pamoja na mambo mengine Rais Samia amesema serikali inafanya tathmini maalumu kwa taasisi hizo za dini ili kubaini zile zinazofanya biashara zichangie kodi ya serikali na zile zinazotoa huduma basi kodi zake zitaangaliwa upya.

error: Content is protected !!