Beki wa kati wa klabu ya Simba Josh Onyango pamoja na kiungo wa mkabaji Sadio Kanoute wataukosa mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United mara baada ya kupata majeraha kwenye mchezo wa ngao ya jamii dhidi ya Yanga. Anaripoti Mintanga Hunda TUDARCo…(endelea)
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii ulipigwa Jumamosi ya Septemba 25, kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na Yanga kufanikiwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0.
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii uliashilia ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2021/22, ambapo leo Simba itashuka dimbani majira ya saa 10 jioni kuwakabili Biashara United kwenye Uwanja wa Karume Mkoani Mara.
Katika kikosi kilichosafiri kwenda mkoani humo, klabu ya Simba ilitoa taarifa ya kutokuwepo kwa nyota hao wawili kwenye mchezo wa leo mara baada ya kubakia Dar es Salaam kwa matibabu Zaidi.
Wawili hao wataungana na Thadeo Lwanga ambaye ataukosa mchezo wa leo kufuatiwa kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita wac Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na hivyo atakaa nje kwa michezo miwili.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wataanza mbio ya kulitetea taji hilo, mara baada ya kulichukua katika kipindi cha miaka minne mfululizo.
Leave a comment