Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Mwinyi ateua viongozi wapya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
Habari za Siasa

Rais Mwinyi ateua viongozi wapya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar
Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameteua wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kuingiza damu changa kutoka Chama cha ADA- TADEA. Anaandika Jabir Idrissa…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Injinia Zena Ahmed Said, Rais amemteua Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Joseph Kazi kuiongoza tume hiyo.

Jaji Kazi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa ZEC, kuchukua nafasi ya Jaji Mkuu mstaafu, Hamid Mahmoud Hamid.

Miongoni mwa walioteuliwa wamo viongozi wa vyama vya siasa.
Miongoni mwao, ni Halima Mohamed Said, mwanachama wa ADA- TADEA.

Halima ambaye kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama hicho, Juma Ali Khatibu, ni mwalimu kwa taaluma, atakuwa mjumbe mwanamke sambamba na Jaji mwingine wa Mahakama Kuu Zanzibar, Aziza Iddi Suwedi.

Khatibu, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, mteuliwa na Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, ameithibitishia MwanaHALISI kuwa Halima ana uzoefu wa ualimu akifundisha sekondari. Ana Shahada ya fani ya Ualimu.

Kupitia taarifa ya Ikulu, Rais Dk. Mwinyi amemteua Ayoub Bakari Hamad, kuwa mjumbe wa Tume ya Uchaguzi, akiwa anarejea baada ya kuwa mjumbe wa Tume iliyosimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, uliomrudisha madarakani Dk. Ali Mohamed Shein, kushika kipindi cha pili cha urais wa Zanzibar.

Naye mwanasheria na wakili maarufu nchini, Awadh Ali Said ameingia kwenye chombo hicho kwa mara ya kwanza. Ayoub na Awadhi, ni wanachama kutoka chama cha ACT-Wazalendo.

Awadh aliwahi kuwa Meneja wa kwanza wa kampeni ya Maalim Seif Shariff Hamad, alipowania kiti cha urais mwaka 1995, ukiwa ni uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.

Awadh ana historia iliyotukuka kwa kuwahi kuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa mwaka 2013, na Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2005.

Tume hiyo ilikuwa chini ya Jaji mstaafu Joseph Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania wakati wa utawala wa Mzee Ali Hasaan Mwinyi.

Wateuliwa wengine kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Idrisa Haji Jecha na Juma Haji Ussi.

Jecha amekuwa ofisa mwandamizi katika tume hiyo; wakati fulani akishika ukaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Mtumishi huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar aliingia kwa mara kwanza kwenye tume hiyo kushika nafasi ya ofisa habari. Ni mwandishi wa habari mwandamizi aliyesomea shahada yake nchini Urusi miaka ya 1980.

Viongozi hao wanatarajiwa kuapishwa Jumatatu ijayo, Ikulu ya Zanzibar, katika hafla itakayoanza Saa 8 mchana.

Uteuzi wa tume mpya umefanywa chini ya msisitizo wa upinzani kutaka Tume Huru kwa kuihuisha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Namba 11 ya mwaka 1985 iliyofanyiwa marekebisho makubwa mwaka 2017.

Wakati huo, Baraza la Wawakilishi likiundwa kwa zaidi ya asilimia 90 ya wajumbe wakiwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya chama cha CUF kilichokuwa na nguvu hata kudai kushinda uchaguzi kwa mara nyengine mwaka 2015.

Kutokana na madai hayo ya kunyang’anywa ushindi, CUF kilikataa kushiriki uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa vile haikuyatambua matokeo ya uchaguzi ikiwemo uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, wa kufuta uchaguzi na matokeo yote.

Madai ya kuhuishwa kwa Sheria ya Uchaguzi yanaenda sambamba na mahitaji ya kujengwa msingi imara wa kimfumo wa kuendesha uchaguzi kusudi kuwe na uhakika wa kufanyika uchaguzi ulio huru, wa haki na utakaotoa matokeo ya kuaminika.

Chama cha ACT Wazalendo ambacho ndicho kilichoshiriki kuundwa kwa serikali ya sasa chini ya Dk. Mwinyi kimewasilisha mapendekezo ya namna tume huru inavyopaswa kuwa.

Msimamo huo unahusisha pia haja ya kutekelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kwa ushirikiano wa Rais Dk. Mwinyi na Maalim Seif, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, kabla ya kufariki dunia Februari 2021.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

Habari za Siasa

ACT: Waongoza watalii wapate maslahi yao inavyostahili

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo kimeitaka serikali kuhakikisha inasimamia maslahi stahiki ya...

Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba ajitosa kuviunganisha vyama vya siasa Burundi

Spread the love  MWENYEKITI wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Prof. Ibrahim...

error: Content is protected !!