May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Mwinyi amwapisha mrithi wa Maalim Seif

Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais ya Mapinduzi Zanzibar, akiapa mbele ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi Ikulu Zanzibar

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, amemwapisha Othuman Masoud Othuman wa chama cha ACT-Wazalendo kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Othuman mwenye miaka 58, ameapishwa leo Jumanne, tarehe 2 Machi 2021, Ikulu ya Zanzibar kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad (77), aliyefariki dunia 17 Februari 2021.

Maalim Seif, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, alihudumu nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais kwa siku 71, tangu alipoapishwa na Rais Mwinyi, 8 Desemba 2020.

Othuman, aliyezaliwa tarehe 7 Februari 1963, Kijiji cha Pandani, Wete visiwani Pembe, amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, enzi ya utawala wa Rais Dk. Ali Momahed Shein.

Rais Mwinyi, amemwapisha Othuman baada ya kumteua jana Jumatatu, kushika wadhifa huo, ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Mara baada ya shughuli ya kumwapisha Othuman kukamilika, lilifuatia tukio la upigaji picha mbalimbali na hakukuwa na hotuba zozote za viongozi, zilizotolewa.

Othuman, anakuwa mtu wa pili kushika wadhifa huo, tangu kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, ambapo aliyekuwa wa kwanza kushika nafasi hiyo, alikuwa Maalim Seif.

Jana Jumatatu, mara baada ya kuteuliwa na Rais Mwinyi, makamu huyo wa Rais, alitoa andishi akizungumzia uteuzi huo.

Ndugu zangu na wenzangu nyote, najua shauku na hamasa zenu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Najua imani yenu kwangu, hata wale waliokuwa wakihoji juu ya uwezo wangu au kufaa kwangu kwa nafasi hii, walifanya hivyo kwa nia safi na hamu ya kupata mtu atakayekidhi haja.

Hakuna anayeweza kukidhi vigezo wala viwango vya Maalim Seif. Hakuna na hatotokea.

Mimi sikuwa nimeshindanishwa na yeyote bali nimetiwa katika mezani na kuonekana sio mzito zaidi, bali ninaelekea kwa yale viongozi wetu wa chama waliyoyaona yatafanana na uwezo wa kuendeleza msingi mzuri na madhubuti ambao mzee wetu Marehemu Maalim Seif kwa kushirikiana na Rais wetu Dk Mwinyi wameujenga.

Kamwe sitojipima mezani ya Maalim daima sitotimia, bali nitajipima katika mezani ya matarajio ya watu wa Zanzibar na hatma ya nchi yao. Shauku na haki ya maendeleo. Haki ya maridhiano, utulivu na mshikamano.

Haki ya kuwa pale wanapostahiki. Haki ya kuwa na fahari na nchi yao. Hayo naamini yatapatikana kwa kumsaidia Rais wetu kujenga misingi imara ya taasisi za umma.

Misingi imara ya uwajibikaji na uadilifu. Misingi imara ya haki za kijamii. Misingi imara ya Sheria na usimamizi wa sheria na misingi imara ya uchumi kwa uwekezaji wa Serikali na ushiriki wenye tija wa sekta binafsi.

Zanzibar ina fursa ya kipekee kwa kutumia rasilimali watu, vipawa na uwezo wa watu wake waliopo ndani na nje. Kinachohitajika ni mashirikiano ya wote, mashirikiano ya dhati.

Sasa tunakwenda mbele kwa pamoja. Nawashukuru kwa namna ya kipekee.

error: Content is protected !!